Propela

aa

million ads

Millionaire  Ads

Tuesday, February 21, 2017

Bodi ya Tazara waziangukia serikali ya Tanzania, Zambia

BODI ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) wameziomba serikali za Tanzania na Zambia kuja na hatua za muda mfupi za kuisaidia mamlaka hiyo kuwa hai.
Hayo yamebainishwa kwenye tamko la bodi hiyo iliyokutana juzi Dar es Salaam, ikijumuisha makatibu wakuu katika wizara za Uchukuzi katika nchi za Zambia na Tanzania lililotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha Tazara, Conrad Simuchile.
Katika kikao hicho, bodi imeafikiana kuchukua hatua za muda mfupi kwa kuomba serikali hizo mbili ambao ndio wenye hisa kuifanya Tazara hai wakati wanaangalia njia mwafaka zaidi na endelevu ya kuipatia fedha mamlaka hiyo ambazo zitafanya mapinduzi makubwa na ya muda mrefu.
“Tunatambua kuwa shughuli za Tazara zimeathiriwa vibaya na kuwapo kwa mtaji mdogo na hivyo kuwapo haja ya kuongeza mtaji ili kuinusuru mamlaka. Bodi inaomba kuja na njia ya muda mfupi wa kuongeza fedha ili kuifanya Tazara iwe hai,” ilisema taarifa hiyo.
Kuhusu mishahara, bodi imetatua tatizo la kuondolewa kwa malipo ya ziada kwa wafanyakazi katika sekta ya utoaji huduma kwa kuanzisha posho na imeiagiza menejimenti kutekeleza ulipwaji wa viwango vipya vya mshahara kulingana na gharama ya ubadilishaji fedha baada ya kufanya makubaliano ya pamoja ya marekebisho hayo.
Hivi karibuni, huduma za usafiri kwa upande wa Zambia zilisitishwa kwa siku kadhaa kutokana na mgomo wa wafayakazi waliotaka kuwapo kwa marekebisho ya mishahara kulingana na kiwango cha kubadilisha dola za Marekani.
Kuhusu ufanisi katika utoaji huduma katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016/2017, bodi imebainisha kuwa Tazara imesafirisha tani 74,122 za mizigo ambayo ni asilimia 31 zaidi ukilinganisha na kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni mwaka 2016 ambapo walisafirisha tani 56,589.
Hata hivyo, kiasi hicho cha mizigo kilichosafirishwa ni asilimia 35.5 ya malengo ya kusafirisha tani 208,602 katika kipindi hicho.
Kwa upande wa treni ya abiria, wamesafirisha abiria 278,019 katika kipindi cha miezi sita ukilinganisha na abiria 207,090, hivyo kufanya kazi hiyo kwa asilimia 34.3.
Kiwango hicho kimezidi kwa asilimia 1.1 ukilinganisha na malengo ya awali ya kusafirisha abiria 275,004. Treni ya safari fupi ya Udzungwa imesafirisha abiria 144,555 ukilinganisha na abiria 108,218 waliosafirisha kipindi kama hicho mwaka uliopita wakati treni inayofanya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam imesafirisha abiria 1,389,590 ukilinganisha na abiria 841,894 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.

0 comments:

Post a Comment