Monday, November 7, 2016
Makonda umenena ujenzi vituo vya polisi
JUZI Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametangaza azma ya mkoa huo kujenga vituo vya polisi vya kisasa zaidi ya 20, ambavyo mara vikikamilika kila kimoja kitakuwa na askari 1,000 kwa wakati mmoja.
Makonda amesema, ujenzi huo tayari umeshaandaliwa Sh bilioni 10 ili kuhakikisha vituo hivyo vinakamilika na kuanza kutumika. Vituo hivyo ambavyo vitakuwa na mfumo bora wa mawasiliano na vitamwezesha mtu mwenye shida kuuliza au kumwulizia ndugu yake popote alipo kujua kama amekamatwa.
Tunaunga mkono mkakati huo wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wa kujenga vituo vipya vya kisasa, ambavyo vitakuwa na mahabusu ya wanawake na wanaume, wenye mahitaji maalumu na kujengwa katika maeneo ambayo yanaongoza kwa uhalifu.
Sisi tunaunga mkono azma hiyo kutokana na ukweli kwamba vituo vingi jijini Dar es Salaam kama si vyote, vipo katika hali mbaya, vibovu, vikachavu, havina ulinzi wa kutosha na vilijengwa zamani na vililenga kutumikia watu wachache kuliko sasa.
Ni ukweli usiopingika kwamba vituo vyetu vya polisi, mfano vya Tandika, Gongo la Mboto, Kigogo, Urafiki, Mburahati, Ukonga na Kituo cha Mwenge, na vingine vingi ambavyo hakuvitembelea Mkuu wa Mkoa Makonda mwishoni mwa wiki, vina hali mbaya kiuwezo, kimajengo, askari na silaha.
Sisi tunaamini kwamba, ujenzi wa vituo hivyo vipya vya kisasa 20, utasaidia kuvifanya viwe imara na kuwa na uwezo wa kutunza silaha na askari wengi, hivyo vitasaidia katika kampeni ya kupambana na wahalifu, jambazi na watumia dawa za kulevya jijini Dar es Salaam na kulifanya jiji hilo kuwa mahali salama zaidi.
Kitendo cha serikali kujenga vituo hivyo, umekuja wakati muafaka kutokana na kwamba hali ya uhalifu, ujambazi na matukio mengine ya kihalifu ya kutumia silaha yamezidi kuongezeka jijini.
Wakati huu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, hata mbinu za wahalifu zimeongezeka na hata wahalifu wenyewe ni watu wenye mbinu nyingi, hivyo ni lazima vituo vya polisi viwe imara kuanzia majengo yake, silaha kubwa pamoja na askari wengi ili kupambana na wahalifu hao.
Ujenzi wa vituo vinne katika kila wilaya za Ubungo, Kinondoni, Temeke, Kigamboni na Ilala, utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya uhalifu na matukio ya kuibiwa silaha vituoni na hata kuwaua askari katika maeneo husika na hivyo kusaidia ulinzi na kuongeza usalama katika jiji zima la Dar es Salaam.
Pamoja na ujenzi huo, wananchi nao wanalo jukumu kubwa la kushirikiana na polisi katika kuwafichua wezi wanaotumia pikipiki zinazoitwa bodaboda, majambazi na wanaotumia silaha pamoja na wauza dawa za kulevya ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Wananchi wanao wajibu wa kutoa taarifa kwa polisi wa vituo husika au vilivyo karibu nao, mara wanapowaona wahalifu au kusikia taarifa za kuwapo wahalifu mahali fulani jijini, ili polisi walioimarishwa kwa silaha na uwingi wao, wapambane nao.
Kama wananchi wataonesha ushirikiano kwa askari kwa kuwapa taarifa za uhalifu, ujambazi na vitendo vingine vya uhalifu, hakika jiji la Dar es Salaam uhalifu, ujambazi na matukio mengine ya kutumia silaha yatapungua.
Sisi tunaipongeza serikali kwa kuamua kujenga vituo vya polisi vya kisasa jijini, lakini pia tunawaomba wananchi watoe ushirikiano kwa polisi katika kutoa taarifa za uhalifu, ili jeshi hilo lidhibiti vitendo hivyo vya uhalifu na kuwakamata wahusika ili kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Tunaipongeza serikali kwa mkakati huo wa kujenga vituo vipya na vya kisasa ambavyo vilikuwa katika mbayana havikulinga na hadhi ya jeshi hilo linalowalinda raia na mali zao, ndiyo maana tunasema azma ya kujenga vituo aliyoitoa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda imekuja wakati wakati muafaka.
0 comments:
Post a Comment