Propela

aa

million ads

Millionaire  Ads

Monday, November 7, 2016

Bunge lammwagia sifa Sitta, laahirishwa

BUNGE limeahirisha shughuli zake hadi leo kutokana na kifo cha aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta huku Mbunge wa Viti Maalumu kutoka mkoani Tabora anakotoka pia Sitta, Munde Tambwe (CCM) akimwaga machozi bungeni. Wabunge wameshtushwa na kifo cha Sitta na kumuelezea katika kipindi cha uongozi wake, ndiye aliyelipa nguvu Bunge kuisimamia serikali, akaboresha maslahi ya wabunge pamoja kusimamia kile alichokiamini bila woga. Hoja ya kuahirishwa kwa Bunge ilitolewa na Munde aliyesimama kuomba Mwongozo wa Spika baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu, akisema “Taifa limepoteza kiongozi mahiri hususan Tabora, Sitta alikuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, la Katiba.” Hata hivyo, kabla ya kumaliza alianza kulia na baada ya sekunde chache akamalizia kwa kutoa hoja ya kuahirishwa kwa Bunge. Pamoja na kutoa hoja hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alikataa kuahirishwa kwa shughuli za Bunge na kusema Kanuni za Kudumu haziruhusu kwani alishastaafu na tayari Ofisi ya Bunge kwa kutambua heshima ya Sitta imegharamia matibabu yake. Kauli hiyo ilipingwa na wabunge wa upande wa upinzani na CCM wakiomba Mwongozo, walisikika wakisema huo ni msiba lazima Bunge liahirishwe na ndipo Zungu akampa nafasi Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT Maendeleo), atoe mwongozo ambaye alisema hakuna Spika mstaafu yaani Adam Sapi Mkwawa na Erasto Mang'enya aliyefariki dunia wakati Bunge likiendelea na shughuli zake. "Bunge linaendeshwa kwa busara na desturi naomba liahirishwe leo, hoja iletwe iamuliwe,” alisema Zitto. Hata hivyo, Zungu alipinga tena na kusema uamuzi unabaki palepale na mazishi yatagharamiwa na Bunge. Kauli hiyo ilizusha kelele na wabunge wengi wakasimama wa upande wa upinzani na CCM huku wengine wakipiga meza wakitaka Bunge liahirishwe. Baada ya kuona kelele ni nyingi, Zungu licha ya kuwa alishamruhusu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 3 wa Mwaka 2016, akaagiza Kamati ya Uongozi ikakutane na baada ya dakika 10 wapeleke jibu ndipo saa 5:12 asubuhi Bunge likaahirishwa kupisha Kamati ya Uongozi ambayo inaongozwa na Spika kukutana. Ilipofika saa 5:50 asubuhi Bunge likarejea na Zungu akatangaza rasmi kuahirishwa kwa shughuli za Bunge hadi leo asubuhi kutokana na kamati hiyo kuona Sitta alikuwa spika na kwa heshima yake na kazi kubwa aliyofanya Bunge lazima liahirishwe. Alitumia Kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge inayosema "....Spika atafanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria nyingine za nchi, Kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa Bunge la Tanzania.” Wakimzungumzia Sitta nje ya Bunge jana, wabunge walieleza kusikitishwa na kifo hicho kwani ni pigo kwa taifa, wabunge na wananchi kutokana na ujasiri aliokuwa nao na kuleta mageuzi kwenye Bunge hasa kwenye kuisimamia serikali. Waziri wa Katiba na Sheria ambaye ni Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe alisema sura ya sasa ya Bunge na uwezo wa kuisimamia serikali imetokana na falsafa yake ya kasi na viwango. “Kifo chake ni pigo kwangu na familia yangu kwani alikuwa kama kaka yangu tuliyeshabihiana kiitikadi na ni pigo kwa Watanzania wanaopiga vita ufisadi,” alisema Dk Mwakyembe ambaye katika Bunge la Tisa likiongozwa na Sitta, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyoshughulikia suala la kashfa ya Richmond ambayo ilisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu wadhifa huo. Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) alisema Sitta ameacha alama kwani ni Spika aliyepandisha hadhi Bunge, kazi aliyofanya kwenye Bunge la Tisa na kuendelea Bunge la 10 itakumbukwa kwenye historia kwani ndiye mabunge bora zaidi. Alisema Sitta ameacha fursa kwa nchi kupata Katiba mpya iliyo bora. Katibu wa Wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza alisema wabunge wa CCM wamepokea kwa mshituko msiba huo na kutoa pole kwa wabunge, familia na Watanzania kiujumla ambapo alisema "Wabunge wa CCM tuliopo bungeni tutapanga namna ya kushiriki msiba huo kuanzia kuupokea mwili kutoka Ujerumani hadi kushiriki msiba wote.” Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alimuelezea Sitta kuwa "alikuwa jasiri, alikuwa na uwezo wa kusimamia anayoyaamini, mzalendo, amefanya mageuzi bungeni na kila alipofanya kazi ameacha alama. Katiba imekamilika kwa asilimia 85 na imebaki kupitishwa tu na hiyo ni kutokana na nguvu yake (Sitta).” Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) alisema Sitta aliwaunganisha wabunge wa Tabora bila kujali itikadi za vyama vyao vya siasa na amemfunza awe kiongozi wa kujenga watu wawe wamoja na aongoze kwa utu, asiwe mwoga kwenye kutenda jambo kwa maslahi ya taifa hata kama jambo litamgharimu. Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige (CCM) alisema Sitta alipokuwa Spika alijali maslahi ya wabunge na akaboresha mishahara, posho, marupurupu na akaanzisha ofisi za wabunge majimboni na Mfuko wa Jimbo. Pia kulianzishwa Mfuko wa Bunge unaojiendeshea shughuli zake badala ya kuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) alimwelezea kiongozi huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa alikuwa jasiri, alitetea haki hata kama ina athari kwa wengine na alisimama kidete kuhakikisha katiba mpya inapatikana. Akizungumzia Sitta ambaye alianza kuwa Mbunge mwaka 1975, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema) alisema "amewajenga wabunge wa CCM na wa upinzani bila kujali kama yeye ni CCM na hata mimi lazima niende kwake kupata ushauri. Alijenga Bunge imara na msingi wa kuisimamia serikali.” Mbunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee (Chadema) alimwelezea Sitta kuwa alikuwa spika wa viwango na katika kipindi chake cha uongozi Bunge halikuweza kuingiliwa na serikali ndiyo maana aliweza kusimamia kushughulikiwa sakata la Richmond na EPA. Kwa upande wa watumishi wa Bunge wameelezea kusikitishwa na kiongozi huyo, ambapo Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Owen Mwandumbya alisema Sitta alipigania maslahi wa ya watumishi wa Bunge kwa kuhakikisha kuwa wanatengenezewa mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Alisema moja ya vitu alivyoamini muda wote ni kwamba kila mtu ana uwezo wa kufanya kazi maadam anawezeshwa vitendea kazi. “Katika moja ya misamiati ambayo hakuipenda kabisa kuisikia masikio mwake ni pamoja na maneno kama ' Tunashughulikia, tupo kwenye mchakato' au namna yoyote ya kutoa majibu yasiyo na ukomo wa utekelezaji wa majukumu,” alieleza Mwandumbya. Awali akisoma taarifa ya iliyotolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Mwenyekiti wa Bunge, Zungu alisema Bunge limepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Spika wa Bunge la Tisa aliyefariki saa 7:50 usiku kwa saa za Ujerumani (saa 09:50 alfajiri nchini) wa kuamkia jana katika Hospitali ya Technical University of Munich alipokuwa anatibiwa. Sitta aliondoka nchini Novemba 3, mwaka huu na kwenda nchini humo kwa ajili ya matibabu ambayo Bunge lilikuwa likigharamia. Zungu alisema Bunge linatoa pole kwa familia hususan Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta (CCM) ambaye ni mke wa marehemu.

0 comments:

Post a Comment