Monday, November 7, 2016
WAPIGA DILI WA CCM HAWAKUMPENDA SITTA
“SIKU zote mimi ni mtu wa viwango na ukweli. Hata wakati nilipokuwa Spika wa Bunge, baadhi ya wakubwa zangu wa kazi hawakufurahishwa na uwazi, viwango na spidi yangu ya kuongoza Bunge.
“Kwa sababu ya baadhi ya wakubwa wangu kutofurahishwa na viwango vyangu, nilistaafishwa Uspika kabla ya muda wangu. Sababu na kisingizio chao, eti huu ni wakati wa Bunge kuongozwa na mwanamke! Hii mmh.”
Hayo ni maneno aliyopata kuyasema Spika wa zamani wa Bunge, Samuel Sitta ambaye jana aliaga dunia katika Hospitali ya Technical University ya nchini Ujerumani, alikokuwa amelazwa akipata matibabu. Kwa mujibu wa familia yake, amefariki kutokana na maradhi ya tezi dume.
Sitta (73) amekuwa kwenye siasa kwa miaka 35 ya maisha yake.
Yapo mambo mengi ambayo yanaweza kuandikwa juu yake, lakini kwa umri wangu nimemjua Sitta akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), lakini umaarufu wake ulikuwa juu zaidi wakati akiwa Spika wa Bunge la Tisa kuanzia mwaka 2005 hadi 2010.
Ni kupitia kaulimbiu yake ya Spika wa Viwango na Kasi ndiyo iliyomfanya mwanasiasa huyo ambaye wakati huo alikuwa Mbunge wa Urambo Mashariki kufahamika zaidi kwa jamii.
Alipendwa na wanaCCM na wapinzani pia kutokana na kuwapa fursa ya kuibua madudu mengi yaliyokuwa yanafanywa serikalini. Pamoja na kupendwa kwake na wapinzani hakuwaachia tu wafanye watakavyo. Zitto Kabwe ni mmoja wa wanasiasa wanaokumbuka namna spika huyo alivyosimamia suala la mbunge huyo kijana kudaiwa kutoa hoja ya uongo dhidi ya mkataba wa mgodi wa Buzwagi.
Zitto alisimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa miezi minne. Mwaka 2010, Sitta alijitokeza tena kuomba kugombea uspika tena huku akiamini kuwa alitaka aendelee na kasi na kiwango alichokianzisha kwenye mhimili huo wa Bunge.
Pamoja na yeye, wengine waliojitokeza kugombea uspika ndani ya chama chake ni aliyekuwa Naibu Spika, Anne Makinda, aliyekuwa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Anna Abdallah na Kate Kamba. Katika kundi hilo, Sitta na Chenge walienguliwa na Kamati Kuu ya CCM na kuwaacha wanawake wawanie nafasi hiyo jambo ambalo lilionekana kutomfurahisha Sitta mwenyewe.
Hatimaye Makinda alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la 10. Baada ya kuenguliwa kwenye kugombea uspika, ndipo Sitta aliibuka na kuwatuhumu viongozi wenzake ndani ya CCM kuwa walishiriki kwenye njama ovu za kumnyang’anya uspika kwa sababu waliogopa spidi na viwango vyake.
Sitta hakuficha hasira zake, alisema hujuma hiyo ililenga kumstaafisha kwa lazima kabla ya muda wake, kwa kisingizio cha wakubwa zake hao kutaka Bunge liongozwe na mwanamke, jambo ambalo alionekana kutoridhishwa nalo.
Katika mambo mengi aliyofanya, Sitta ndiye aliyeunda Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza ufisadi kuhusu ukodishaji wa mitambo ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond. Kampuni hiyo ilipewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura baada ya nchi kuingia kwenye ukame na hivyo kusababisha mabwawa ya kuzalisha umeme yakawa yamekauka.
Hata hivyo, kampuni hiyo haikutimiza ahadi yake ya kuzalisha umeme huo wa dharura. Tume hiyo aliyoiunda chini ya uenyekiti wa Dk Harrison Mwakyembe ndiyo ilifanya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu wadhifa wake baada ya kutuhumiwa na kamati hiyo kuwa alihusika kwa namna moja kuipigia debe kampuni hiyo ya Marekani kupata zabuni hiyo wakati haikuwa na uwezo. Wakati wa uongozi wake ndani ya Bunge, Sitta alijipambanua kuwa mpinga vitendo vya ufisadi.
Aliahidi kupambana na mafisadi pasipo na woga kwa kuwa aliamini ndiyo nia nzuri ya kuliokoa taifa.
Ni kutokana na msimamo huo akajulikana kama kiongozi wa kundi la wabunge wanaopinga ufisadi. Pamoja na yeye Sitta, kwenye kundi hilo alikuwemo aliyekuwa Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, aliyekuwa Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (sasa marehemu), Mbunge wa Kyela, Dk Mwakyembe, aliyekuwa Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango na aliyekuwa Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii, kwa kutaja wachache.
Alipokosa uspika, Sitta aliteuliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wadhifa ambao aliendelea nao hadi mwaka 2014. Akiwa kwenye wadhifa huo, Sitta alizidi kulia na ufisadi, rushwa na wizi uliokuwa unaendelea kuangamiza uchumi wa taifa.
Akiwa katika ziara ya kikazi mjini Bukoba, mwanasiasa huyo alisema mtandao wa walarushwa nchini ni mkubwa na watu wachache wameupenyeza katika Serikali, CCM na sasa umeanza kulitikisa hata Bunge. Alisema kuna kundi la wanasiasa ambao waliitumia nafasi zao kujineemesha ikiwemo kufanya biashara.
Bunge la Katiba Katika maisha yake, Sitta alipata fursa ya kuchaguliwa kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba akisaidiwa na Samia Suluhu Hassan. Alichaguliwa Machi 2014 akiwa na jukumu la kuliongoza Bunge hilo kuwapatia Watanzania Katiba mpya.
Aliliongoza Bunge hilo katika mazingira magumu baada ya baadhi ya wajumbe hasa wa kutoka vyama ya upinzani kulisusa kwa maelezo kuwa CCM tayari ilikuwa na Katiba yake wanayoitaka na hivyo kupuuzia maoni ya wapinzani.
Pamoja na mtikisiko huo, Sitta alifanikisha kutungwa kwa rasimu mpya ya Katiba inayosubiri kupigiwa kura ya maoni na Watanzania. Ajitosa Urais Sitta ni miongoni mwa wanasiasa wachache ambao waliaminiwa na marais wanne na kumteua kufanya nao kazi.
Alifanya kazi awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere hadi Awamu ya Nne ya Rais Kikwete ambaye hadi anahitimisha uongozi wake alimteua Sitta kuwa Waziri wa Uchukuzi. Hiki kilimpa ujasiri Sitta kuamini kuwa alikuwa anafaa kuwa Rais wa Tanzania. Aliamini katika uadilifu na alitamani kuiona Tanzania inakuwa na jopo la kuhoji viongozi na wananchi wawe na fursa ya kuwachambua.
Aliamini kuwa Tanzania ilihitaji mfumo ambao utajenga mazingira ya kuwa na viongozi waadilifu katika ngazi zote.
Sitta aliamini kuwa hiyo itaepusha mfumo unaoonekana sasa wa viongozi kwenye ngazi mbalimbali kuishi kiujanjaujanja, kujinufaisha na kutojali athari kwa uchumi wa nchi na Watanzania kwa ujumla.
Wakati Rais Jakaya Kikwete alipokuwa anakaribia kumaliza muda wake wa uongozi, mwanasiasa huyo mkongwe alitoa mwito kwa wasomi na Watanzania wote kutowaunga mkono wanasiasa walioihujumu nchi kupitia mikataba mibovu ya kifisadi ambao wangejitokeza kuwania urais.
Kwa kuwa yeye alishajipima na kuona anafaa kuwa Rais, alichukua fomu ya kugombea urais na akawa miongoni mwa makada zaidi ya 30 wa Chama Cha Mapinduzi waliojitokeza kuwania urais kwa tikei ya chama hicho kikongwe.
Aliwania urais, lakini akiwa anaamini kuwa Bernard Membe, Dk John Magufuli, Dk Mwakyembe na yeye mwenyewe miongoni mwao mmoja wao anafaa kuwa Rais. Hivyo jina lake lilivyokatwa marafiki zake wawili Membe na Magufuli walibaki.
Aliridhika na hatua hiyo na wakati wa kampeni alijitokeza kumpigia debe mgombea wa CCM, Dk Magufuli. Sitta hakugombea ubunge wa Urambo Mashariki (sasa Urambo), ila aliendelea kutamani kuwemo kwenye Bunge na hivyo aligombea tena uspika wa Bunge. Safari hii hakuwa na mvuto sana kama aliokuwa nao mwaka 2010.
Alikatwa tena na Kamati Kuu na baada ya hapo, Sitta alitangaza kustaafu siasa. Tangu wakati huo hakusikika tena. Kuumwa hadi mauti Septemba mwaka huu, ugonjwa wa Sitta uliripotiwa na baadhi ya vyombo ya habari kuwa mwanasiasa huyo mkongwe alikuwa anasumbuliwa na miguu.
Baadaye viongozi wakuu wa nchi Rais John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa walikwenda nyumbani kwake kumjulia hali. Baada ya hali yake kuendelea kudhoofu, Septemba mwishoni Sitta alipelekwa Ujerumani kwa matibabu zaidi.
Alirejea nchini, kabla ya kupelekwa tena nchini humo ambako hadi mauti yanamkuta usiku wa kuamkia jana kiongozi huyo alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Technical University ya mjini Munich, Ujerumani. Ukweli ni kwamba Sitta aliyezaliwa Desemba 18, 1942 ni kiongozi aliyeacha historia katika nchi yake.
Ni kiongozi aliyekamilisha majukumu kwa Mungu wake, kwa familia yake na kwa taifa lake. Mambo aliyoyapigania ndio leo Rais Magufuli anayasimamia. Kwangu mimi Sitta alikuwa ni mwanasiasa wa mfano anayepaswa kuigwa na wanasiasa vijana.
0 comments:
Post a Comment