Saturday, March 25, 2017
Chadema kutumia Bunge kufafanua hali ya siasa nchini
Thursday, March 23, 2017
Kuhusu Nape Nnauye, CUF kutangaza hatua nzito
TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI
Chama cha Wananchi CUF kimepokea taarifa ya hatua ya Rais Magufuli kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na kumuondoa Mheshimiwa Nape Nnauye katika nafasi ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa mshtuko na masikitiko makubwa.
Mhe. Nape ameondolewa kwenye Baraza la Mawaziri kibabe na bila aibu kutokana na kusimamia Haki, Uhuru, Uwajibikaji, Nidhamu na Maadlili ya uendeshaji wa vyombo vya habari nchini jambo ambalo ni jukumu la msingi la Wizara yake.
Sote tunatambua kwamba Utenguzi huo unatokana na Mhe. Nape kufuatilia tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuvamia kituo cha Clouds Media Group kinyume na taratibu, maadili na Nidhamu ya utendaji wa majukumu yake. kitendo hicho pia ni kosa la jinai lisilovumilika.
Kwa niaba ya Chama cha Wananchi CUF, napenda kutumia fursa hii kulaani mwenendo wa Rais Magufuli wa kuitumia nafasi yake kwa namna inayokosa BUSARA na HEKIMA ya uongozi kwa TAASISI ya URAIS.
Kitendo cha Rais kumlinda mtuhumiwa ambaye amefanya makosa ya wazi kabisa kinadhihirisha namna Rais asivyo na utayari wa dhati na uwezo wa kusimamia nidhamu ya watendaji serikalini.
Huko nyuma na mara kadhaa, Rais Magufuli alichukua hatua za haraka sana kuwafuta kazi watumishi na watendaji wa serikali waliofanya makosa madogo mno hata kama ilikuwa ni kimatamshi tu au maamuzi ya bahati mbaya.
Mifano mizuri ni pamoja na Mhe. Anne Killango (aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga), Dr. Mwele Malecela (aliyekuwa anaongoza taasisi muhimu ya utafiti wa magonjwa ya binadamu), Wilson Kabwe (Mkurugenzi wa Jiji la Dar Es Salaam) ambaye alituhumiwa mkutanoni na kufukuzwa hapo hapo bila kuwepo wala nafasi ya kujitetea.
The Civic United Front (CUF) inashangazwa na maamuzi ya sasa ya Rais Magufuli ya kumlinda mtuhumiwa wa makosa makubwa na ya wazi kabisa na kisha kumfukuza kazi Waziri aliyekuwa akitekeleza wajibu wake ili kulinda heshima ya serikali.
Kwa kitendo hiki cha Rais, CUF inaungana na watanzania wote kuamini kuwa Rais Magufuli hana nia njema ya kurejesha nidhamu serikalini, na kwamba yuko tayari kuwalinda vijana wake wachache kuliko kuilinda serikali na heshima ya nchi na Taasisi ya Urais. Rais anashusha hadhi ya Ikulu na sasa ikulu imegeuka kuwa mtetezi mkuu wa watumishi waovu wa umma.
CUF itatangaza hatua nzito hapo baadaye, kwa niaba ya chama natumia fursa hii kumfariji na kumtia nguvu Mhe. Nape kwa ujasiri aliouonyesha na kusimamia kile ambacho ni haki kwa Taifa, wananchi na sekta ya habari.
Namuomba asirudi nyuma kutetea haki za watanzania wote na kamwe asikatishwe tamaa na kitendo hicho kilichokosa utu na heshima, na kujali mchango mkubwa wa kisiasa ndani ya Chama chake na serikali ya awamu ya Tano.
CUF inaungana na watanzania wote kulaani kitendo hicho na kwamba tutakutana pia na vyama washirika katika UKAWA ili kuamua hatua kubwa za pamoja dhidi ya ukosefu wa haki na Demokrasia nchini na matumizi mabaya ya mamlaka.
"CUF NI TAASISI IMARA YENYE VIONGOZI MAKINI"
HAKI SAWA KWA WOTE
JULIUS MTATIRO
MWENYEKITI WA KAMATI YA UONGOZI
CUF-TAIFA.
23 Machi, 2017.
Tuesday, March 21, 2017
Wabunge CAF Mbaroni Kwa Tuhuma Za Mauaji
WAKATI Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), likitoa maazimio yake ikiwemo kubariki kuvuliwa kufurushwa kwa kuvuliwa uanachama vigogo wake, wabunge wawili wa chama hicho wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani kwa tuhuma za kutishia kumuua mbunge mwenzao.
Akizungumza na MTANZANIA jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazarto Mambosasa, alisema kuwa wabunge hao wamehojiwa kutokana na tuhuma za kudaiwa kumtishia kumuua Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF).
Viongozi hao wa CUF wamekuwa na mvutano ndani ya chama kwa muda mrefu sasa na kupelekea kuzaliwa kwa makundi mawili likiwemo linalomuunga mkono Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama, Profesa Ibrahim Lipumba na lile linalomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.
Kamanda Mambosasa, alisema baada ya mahojiano na wabunge hao jeshi hilo liliwaachia huru ili waweze kuendelea na majukumu yao na kutakiwa kufika polisi pale watakapohitajika.
“Ni kweli tumewahoji sababu kubwa ni kumtishia kumuua Mbunge mwenzao Sakaya ila tumewahoji tu na kuwaachia waendelee na shughuli zao,’’ alisema
Akizungumzia Sakata hilo, nje ya Kituo cha Polisi, Katibu wa wabunge wa CUF, Juma Kombo Hamad, ambaye pia ni Mbunge wa Wingwi, alisema wabunge hao walikamatwa kutokana na taarifa zilizotolewa na Sakaya kuhusu kutishiwa maisha ambapo alisema hayo ni masuala la kisiasa.
“Haya ni mambo ya kisiasa tu yakataa vizuri na maisha yataendelea,’’ alisema Juma
Jana Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro alitangaza maazimio la kikao cha Baraza Kuu laUongozi lililoketi Visiwani Zanzibar ambapo kikao hicho kilibariki kuvuliwa uanachama kwa vigogo wake saba ambao, ni Mohamed Habibu Mnyaa, Haroub Shamis, Mussa Haji Kombo, Khalifa Suleiman Khalifa.
Sunday, March 19, 2017
ACT Wazalendo Wamkomalia Rais Magufuli Suala La Katiba Mpya
Chama cha ACT Wazalendo kimemtaka Rais John Magufuli ashughulikie suala la upatikanaji wa Katiba mpya ya Tanzania ambayo mchakato wake ulikwama tangu mwaka 2014 licha ya kufikia katika hatua ya Katiba Pendekezwa.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Msafiri Mtemelwa amesema wao kama chama cha siasa wanamtaka Rais Magufuli kuendelea na mchakato wa kuwapatia watanzania wanyonge Katiba bora kwa kuanzia pale rasimu ya pili ya Jaji Joseph Sinde Warioba ilipoishia.
"Rais Magufuli aanzie na Rasimu ya Jaji Warioba ambayo ilikuwa inatoa nguvu kwa wananchi kuwawajibisha viongozi wao pale wasipotekeleza wajibu wao kulingana na nafasi walizo nazo". Amesema Mtemelwa.
Mtemelwa ameongeza pia "Wakati nchi yetu ikijiandaa kuwapata wawakilishi wapya katika Bunge la Afrika ya Mashariki, Chama cha ACT Wazalendo, tunamuomba Rais Magufuli na tunamkumbusha umuhimu wa watanzania kuwa na Katiba bora itakayoamua maslahi ya nchi katika mfumo ulio rasmi mbali na matakwa ya mtu mmoja pale atakapokuwa anajisikia kufanya hivyo."
Pia amewaomba wadau mbali ikiwemo viongozi wa dini, na taasisi mbalimbali kuweka mkazo katika suala hilo kwa kuwa Katiba iliyo bora itamnufaisha kila mmoja katika jamii
Friday, March 17, 2017
Vigogo wa presha inapanda, presha inashuka sakata la Panga la CCM Zanzibar
HAMKANI si shwari tena! Hivyo ndivyo inavyoelezwa kuhusiana na hali ya hofu inayodaiwa kuwakumba baadhi ya makada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar.
Hali hiyo inatokana na kuundwa kwa kamati maalumu ya kufuatilia mwenendo wa kimaadili wa baadhi ya makada wanaotuhumiwa kukiathiri chama hicho wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
Jumamosi iliyopita, CCM kupitia kamati yake ya maadili na usalama iliwachukulia hatua kali baadhi ya wanachama wake waliohusishwa na makosa mbalimbali ya kimaadili, ikiwamo wengine kufukuzwa uanachama.
Wanachama waliofukuzwa ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida.
Wengine ni wenyeviti wa mikoa wa chama hicho, Jesca Msambatavangu (Iringa), Christopher Sanya (Mara) na Erasto Kwilasa wa Shinyanga.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema CCM imeunda pia kamati ndogo itakayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, kuangalia hali ya kisiasa na kufanya tathmini ya uchaguzi Zanzibar.
Kamati hiyo ambayo pia itawabaini wanachama waliokiuka maadili, inaundwa pia na aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Amiri Kificho, Daud Ismail, Shamsi Vuai Nahodha, Dk. Maua Abeid Daftari, Stephen Wasira na Zakia Meghji.
Katika uchunguzi wake uliohusisha mahojiano na baadhi ya makada wa chama hicho visiwani Zanzibar, Nipashe imebaini kuwa kuundwa kwa kamati ya Mangula na rejea ya kile kilichowakuta kina Simba na Madabida, kumezua hofu kubwa kwa baadhi ya makada wao wanaoonyoshewa vidole kwa tuhuma za ukiukaji wa maadili ya chama na usaliti wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Imeelezwa kuwa baadhi ya wale walio na hofu ni pamoja na wale wanaotuhumiwa kuwa na uswahiba na viongozi wa mahasimu wao wakuu, Chama cha Wananchi (CUF), akiwamo Maalim Seif Shariff Hamad aliyekuwa akichuana na Rais Dk. Ali Mohamed Shein.
“Kama ilivyokuwa Bara, huku (Zanzibar) wapo pia waliokuwa wameng’ang’ania kubaki kwenye kambi za watia nia waliokatwa majina yao wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM hata baada ya Magufuli kupitishwa.
Hawa pia wamejawa hofu kwa sasa,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe.
Aidha, chanzo kingine kilibainisha kuwa miongoni mwa makada waliojawa hofu ya kukutwa na ‘panga’ baada ya uchunguzi wa kamati ya Mangula ni pamoja na wale ambao kauli na matendo yao yaliashiria kutomuunga mkono Dk. Shein.
“Wapo pia walioiweka CCM katika wakati mgumu kipindi cha uchaguzi ule uliofutwa wa Oktoba 25, 2015 kwa sababu nyendo zao ziliashiria kumuunga mkono Maalim Seif.
Hawa pia wamejawa hofu kuhusiana na hatima yao ndani ya CCM,” kilieleza chanzo hicho.
Dk. Shein na Maalim Seif walichuana vikali katika uchaguzi mkuu wa awali uliofanyika Oktoba 25, kabla ya kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutokana na kile alichoeleza kuwapo kwa kasoro nyingi.
Hata hivyo, CUF ilipinga madai ya Jecha na kumtuhumu kuvuruga uchaguzi huo ili kuiokoa CCM iliyokuwa ikidaiwa kuzama kutokana na Maalim Seif kuelekea kushinda.
Katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka jana, CUF ilisusia kwa madai kwamba haukuwa halali hivyo ZEC kumtangaza Dk. Shein kuwa mshindi baada ya kupata asilimia 91 ya kura halali zilizopigwa.
NAIBU KATIBU MKUU ANENA
Akizungumzia kuundwa kwa kamati ya Mangula na hofu ya kutimuliwa baadhi ya wanachama, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai, alisema hakuna sababu kwa mwanachama yeyote mtiifu kuwa na hofu na kwamba anapongeza kilichofanyika kwa sababu ni uamuzi wa busara wenye lengo la kuimarisha chama.
Vuai alisema hatua za kuimarisha chama chao Bara zimeshachukuliwa, hivyo ni busara kwa jambo hilo kufanyika pia visiwani Zanzibar.
“CCM yote ni moja, kilichofanyika Bara kwa lengo la kujenga na kukiimarisha chama ni vyema na Zanzibar kikafanyika pia,” alisema.
Aidha, aliwashauri wanachama wenzake kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo ndogo ya Mangula ili ifanikishe malengo yake.
Katibu wa Oganaizesheni na Idara Maalum ya CCM Zanzibar, Haji Mkema Haji, alisema kamati ya Mangula inapaswa kupewa ushirikiano wa kutosha kwa sababu ni muhimu kwa mustakabali wa chama.
Alisema kamati hiyo ikifanikisha vyema kazi yake, maana yake mambo yote yenye upungufu yatabainika na hatua kuchukuliwa kwa nia ya kuiimarisha CCM.
Kada mwingine wa CCM, Mohammed Said Mohammed, alisema tayari wasaliti wa chama kwa upande wa Bara wamechukuliwa hatua, hivyo ni wakati muafaka kwa hatua kama hizo kuchukuliwa Zanzibar ambako pia kuna wanachama wanaokirudisha nyuma chama kutokana na usaliti wanaoufanya.
Mohammed ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae, alisema badala ya wahusika wa vitendo vya usaliti kutapatapa kwa hofu, jambo la muhimu kwao ni kujiandaa kwa lolote kwa sababu ni lazima kamati hiyo itawabaini kupitia uchunguzi wake.
Lowassa machana JPM
WAZIRI Mkuu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, amemwomba Rais Dk. John Magufuli kufuta kauli yake ya kuwazuia wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kushirikiana na wabunge wa upinzani.
Akizungumza jana katika ziara viongozi wa Chadema katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, Lowassa alisema kauli hiyo Rais Dk. Magufuli inabomoa misingi ya amani iliyojengwa na waasisi wa taifa letu.
'”Namuomba Rais (Magufuli) aondoe kauli ile aisahihishekauli hiyo na nawaomba watanzaniatukatae kugawanywa…tusikubali nchi hii ni yetu sote hakuna mtu mwenye haki miliki hapa ikienda vibaya tunaangamia wote ikienda vizuri tunafaidi wote kwahiyo tukatae,” alisema
Alisema Watanzania wamekuwa wakiishi bila ya kubaguana kwa misingi ya dini, rangi au ukabila na kukumbushia kauli iliyowahi kutolewa na baba wa taifa kuwa ubaguzi ni sawa sawa na kula nyama ya mtu, ukishakula hutotaka kuiacha.
Mjumbe wa huyo wa Kamati Kuu alisema hali ya maisha imezidi kuwa ngumu, huku bei ya bidhaa ikizidi kupanda kila siku.
Kutokana na hali hiyo alisema CCM kiliiba sera ya Chadema, ikiwemo elimu bure, lakini imeshindwa kuitekeleza.
“'waliiba sera na ilani yetu ya uchaguzi, lakini kwa kuwa hawakujiandaa wamefanya hali kuwa ngumu sana,” alisema
Katika kikao hicho cha ndani cha kuimarisha chama, Lowassa ameeleza tatizo la ajira linavyozidi kuwa kubwa na kuongeza kuwa mipango mibovu imesababisha sekta binafsi kuyumba, huku makampuni kadhaa na shughuili nyingine za kutoa ajira zikifungwa na kusababisha ongezeko kubwa la wasiyo na ajira.
Kuhusu ushirikiano miongoni mwa vyama vya upinzani, Lowassa alisema Ukawa ni muhimu kuliko wanavyoweza kudhani kwani muunganiko wa vyama vya siasa katika karne hii ni jambo la muhimu.
“Kikubwa cha kuzingatia ni umoja na mshikamano. Watanzania wana imani kubwa sana na chadema kwa sasa na kama kuna mtu anatafuta chama mbadala cha kuhamia basi ni Chadema,” alisema
Wednesday, March 15, 2017
SOPHIA SIMBA AINGIA KATIKA REKODI HII MPYA CCM
Licha ya ukweli kwamba wajumbe watatu wa Kamati Kuu ya CCM walitoka nje kujitenga na uamuzi wa chombo hicho, Sophia Simba ndiye anayeangaliwa zaidi baada ya Halmashauri Kuu ya chama hicho kuamua kumvua uanachama tofauti na wenzake.
Emmanuel Nchimbi, ambaye sasa ni balozi wa Tanzania nchini Brazil, amepewa onyo kali, wakati mjumbe mwingine wa Kamati Kuu, Adam Kimbisa amesamehewa.
Simba, mwanasiasa mkongwe aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) na ambaye amewahi kuongoza wizara mbili tofauti, anaingia kwenye orodha ya vigogo wa juu wa CCM waliowahi kuvuliwa uanachama kwa tuhuma tofauti.
Wengine ni Maalim Seif Sharif, Katibu mkuu wa CUF ambaye alikuwa mwanzilishi wa kikundi cha kupambania demokrasia cha Kamahuru ambacho baadaye kiliunganishwa na chama cha Civic United Front (CUF) ambacho kimejijenga kama chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar.
Kada mwingine ni Shaaban Mloo ambaye alifukuzwa CCM mwaka 1988 wakati hali ya kisiasa ilipochafuka Zanzibar. Kama ilivyokuwa kwa Maalim Seif, baadaye Mloo alijiunga na chama kipya cha upinzani kilichoitwa Kamahuru.
Mansoor Yusuf Himid ni kigogo mwingine aliyevuliwa uanachama wa CCM kutokana na misimamo yake. Mansoor, ambaye alikuwa mwakilishi wa Kiembesamaki, pia aliwahi kuwa mweka hazina wa CCM-Zanzibar na Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi wakati wa Serikali ya Dk Amani Karume na Dk Ali Mohamed Shein kabla ya kutimuliwa.
Kauli ya Lema kuhusu wabunge CCM waliokwenda kumsalimia gerezani kuitwa wasaliti
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameibuka na kueleza kushangazwa na kauli ya Rais Dk. John Magufuli kwamba wabunge wa CCM waliotaka kwenda kumwona gerezani walikuwa wasaliti.
Lema alisema anatarajia Spika wa Bunge, Job Ndugai, atatoa msimamo juu ya kauli ya kiongozi huyo wa nchi.
Kauli hiyo ya Lema imekuja siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuripotiwa na chombo kimoja cha habari kwamba alishangazwa na hatua ya baadhi ya wabunge wa CCM waliounda kamati ya kutaka kwenda kumtembelea Lema gerezani.
Katika mkutano wake na wabunge hao juzi uliofanyika Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma, Rais Magufuli alisema amekuwa akielezwa kuwa kamati hiyo ilikuwa imepanga safari za kutaka kwenda kumwona Lema alipokuwa gerezani jambo ambalo alilifananisha ni sawa na usaliti kwa chama chake.
Katika taarifa aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, Lema alisema kitendo cha wabunge hao kutaka kumtembelea si usaliti bali ni upendo ambao ni muhimu kwa binadamu yeyote pale anapokuwa na matatizo.
Lema alikaa gerezani kwa muda wa miezi minne kwa kukosa dhamana kutokana na mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.
“Mheshimiwa Rais Magufuli nakusalimu. Nimetoka gerezani hivi karibuni ambako nilikuwa huko kwa zaidi ya miezi minne kwa kunyimwa masharti ya dhamana kwa dhamana iliyokuwa wazi.
“Nimeona kwenye vyombo vya habari leo kwamba wale wabunge waliokuwa wanataka kunisalimia nilipokuwa magereza ni wasaliti wa chama cha CCM.
“Mheshimiwa Rais wengi walinisalimia wakiwemo wachungaji, masheikh, wabunge na viongozi mbalimbali, sidhani kama hatua hii ilikuwa ni usaliti isipokuwa upendo ambao ni muhimu kwa binadamu yeyote pale anapokuwa na matatizo.
“Mheshimiwa Rais nimeogopa sana kwa kauli hii, je Taifa linakwenda wapi? Hivi kweli sisi wabunge ni maadui? Kama viongozi tutafikiri utengano ni moja ya njia ya kuimarisha vyama vyetu, bila shaka tutakuwa tunalitendea Taifa ubaya,” alisema Lema.
Mbunge huyo alisema dhambi hiyo ikikomaa ni wazi kwamba lugha za kidini, ukanda na ukabila hazitaacha kukomaa.
Alisema ni muhimu sasa wakajenga utamaduni wa kuhimiza mshikamano wa kitaifa bila kujali itikadi kama kweli wanapenda masikini na wanyonge.
“Nawaomba wabunge wenzangu walionijali wakati niko gerezani wasijisikie vibaya kwani walifanya jambo jema na muhimu kwa wakati muhimu sana katika maisha yangu ninatarajia kuwa Spika wa Bunge atatoa neon juu ya kauli hii ya Rais.
“Mheshimiwa Rais wakati wa msiba wa Christina Lissu dada yake na Tundu Lissu, nilikuona katika msiba ule wewe na mama yetu mke wako, je wewe ulikuwa unasaliti chama chako?
“Meshimiwa Rais neno la Mungu linasema wapendeni maadui zenu, waombeni wanaowadhi, wabarikini wanaowaonea kwani kufanya hivi ni kuishi kwa thawabu za Mwenyezi Mungu,”alisema Lema.
Mbunge huyo alisema pamoja na hali hiyo ya kuzuiwa lakini aliwashukuru wabunge wa CCM kwa kwenda kumjulia hali, akiwa nyumbani kwake baada ya kutoka gerezani.
“Sina la kusema katika hili kama Rais alikuwa anajua hawakuja kuniona gerezani lakini niwashukuru wabunge wa CCM wote waliokuja kunijulia hali nyumbani. Sisi kama nchi tunatakiwa kuwa na umoja badala ya kuanza kubaguana kwa itikadi zetu za vyama.
“Mdogo wangu wa kike amepata mchumba lakini familia ya huyo mchumba wake inatokana na CCM je tuvunje vikao vya harusi kwa sababu ya tofauti ya vyama?
“Jibu ni hapana sisi ni Watanzania ni lazima tuishi kwa kupenda na kwa umoja kama ambavyo utamaduni wetu unatutaka na si vinginevyo,” alisema.
Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka jana mjini Dodoma nje ya viwanja vya Bunge na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Novemba 4 mwaka jana akikabiliwa na kesi mbili namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.
Katika kesi ya kwanza ya jinai namba 440, anadaiwa kati ya Oktoba 22 mwaka jana maeneo ya Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro, katika mkutano wa hadhara alitoa maneno yenye kuleta tabaka miongoni mwa jamii kwa kutoa matamshi yenye chuki, kuibua nia ovu kwa jamii.
Katika kesi ya pili namba 441, alidaiwa kwamba, Oktoba 23, mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Shule ya Sekondari Baraa, Lema alitoa maneno kuwa:
“Kiburi cha Rais kisipojirekebisha, Rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu, nimeota Mwaka 2020 haitafika Mungu atakuwa ameshamchukua maisha yake,”.
Februari 27, mwaka huu, Mahakama ya Rufaa Tanzania ilifuta rufaa mbili za Jamhuri dhidi ya Lema baada ya mawakili wa Serikali kuieleza mahakama hiyo kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), hana nia ya kuendelea na rufaa, hivyo kuiomba mahakama kuzifuta rufaa hizo zilizokuwa zinahusu dhamana ya mbunge huyo.
Cuf, Maalim wakesha wakilinda ofisi Zanzibar
WAKATI Kamati ya Utendaji ya Taifa ya Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Profesa Ibrahim Lipumba, ikiendelea na vikao vyake Dar es Salaam, wafuasi zaidi ya 100 wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad wamekuwa wakikesha kulinda ofisi za Makao Makuu Zanzibar.
Hatua hiyo imekuja baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita, Profesa Lipumba kutangaza uteuzi wa wakurugenzi wa upande wa Zanzibar na kuahidi kwenda kuwakabidhi ofisi wiki hii Visiwani humo.
Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA imeshuhudia kundi la wanachama hao wa CUF Zanzibar wanaomuunga mkono Maalim Seif wakilinda ofisi za chama hicho zilizopo Mtendeni na Vuga kwa lengo la kuwazuia wakurugenzi hao.
Hatua hiyo imekuja baada ya Maalim Seif kuwataka wafuasi wake juzi mjini Unguja kwamba wawe tayari kulinda ofisi za chama hicho na kupinga uteuzi wa wakurugenzi hao, huku wakiwaita ni feki.
Alisema hila zinazofanywa na Profesa Lipumba ni za makusudi, huku akisema jambo la muhimu ni kuhakikisha wanachama na viongozi wote wasiokubaliana naye wanaungana ili kuhakikisha kuwa hakuna uovu ama ukiukwaji wa sheria utakaofanywa ndani ya chama hicho.
“Ni lazima tulinde chama pamoja na viongozi wake na si vinginevyo, CCM wamekuwa wakifanya kila aina ya majaribu dhidi ya CUF kwa lengo la kumpotezea muda Maalim Seif, ila sisi kama wanachama katu hatukubali.
“Tutasimama imara kulinda kila aina ya mali na hata viongozi, lakini si kuwaruhusu hao wanaoitwa wakurugenzi wa Bwana Yule (Lipumba) kuingia hapa. Ninarudia tena, kama wakithubutu kuingiza hata pua habari yao wataipata,” alisema Masoud Salim Faki ambaye ni mwanachama wa CUF.
MTANZANIA ilimtafuta Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya, ambaye alisema kuwa kauli ya Katibu Mkuu wake Maalim Seif ni ya kujihami na yenye hofu dhidi ya jambo fulani.
“CUF ni taasisi na ina ofisi mbili, moja ipo Zanzibar Mtendeni na Dar es Salaam Buguruni na Katiba inaeleza kuwa kiongozi yeyote wa chama ana haki ya kufanya kazi katika eneo lolote.
“Tunazo taarifa kuwa amechukua vijana kutoka shamba kama 100 ambao tangu jana (juzi) wamekuwa wakilinda ofisi ya Vuga na Mtendeni jambo ambalo anawapotezea muda tu hawa vijana,” alisema Sakaya.
Kutokana na hali hiyo, alisema wao wameendelea na vikao vya kawaida vya kuimarisha chama kuanzia juzi na jana ambapo wakurugenzi wote wanaotambulika kwa mujibu wa Katiba wamehudhuria.
Alisema ofisi za chama haziwezi kuwa kama mali au kampuni ya mtu binafsi kwani siku zote wenye mali zote huwa ni wanachama na si vinginevyo.
“Wakurugenzi walioteuliwa wataendelea na majukumu yao kwa upande wa Zanzibar na hata Bara maana hufanya kazi siku zote kwa pamoja na eneo lolote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyoelekezwa kwa mujibu wa Katiba ya CUF,” alisema Sakaya.
Wiki iliyopita, Profesa Lipumba alitangaza uteuzi wa wakurugenzi wapya na manaibu wao ambao ni Nassor Seif (Mipango na Uchaguzi), Mbunge wa zamani wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Kurugenzi ya Mambo ya Nje), Haroub Mohamedi Shamis (Naibu Fedha na Uchumi), Masoud Ali Said (Naibu Habari na Uenezi) na Thiney Juma Muhamed akiteuliwa kuwa Kamanda wa Blue Guard Tanzania.
Lema ashitushwa na JPM
MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameibuka na kueleza kushangazwa na kauli ya Rais Dk. John Magufuli kwamba wabunge wa CCM waliotaka kwenda kumwona gerezani walikuwa wasaliti.
Lemsa alisema anatarajia Spika wa Bunge, Job Ndugai, atatoa msimamo juu ya kauli ya kiongozi huyo wa nchi.
Kauli hiyo ya Lema imekuja siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuripotiwa na chombo kimoja cha habari (si Mtanzania) kwamba alishangazwa na hatua ya baadhi ya wabunge wa CCM waliounda kamati ya kutaka kwenda kumtembelea Lema gerezani.
Katika mkutano wake na wabunge hao juzi uliofanyika Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma, Rais Magufuli alisema amekuwa akielezwa kuwa kamati hiyo ilikuwa imepanga safari za kutaka kwenda kumwona Lema alipokuwa gerezani jambo ambalo alilifananisha ni sawa na usaliti kwa chama chake.
Katika taarifa aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, Lema alisema kitendo cha wabunge hao kutaka kumtembelea si usaliti bali ni upendo ambao ni muhimu kwa binadamu yeyote pale anapokuwa na matatizo.
Lema alikaa gerezani kwa muda wa miezi minne kwa kukosa dhamana kutokana na mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.
“Mheshimiwa Rais Magufuli nakusalimu. Nimetoka gerezani hivi karibuni ambako nilikuwa huko kwa zaidi ya miezi minne kwa kunyimwa masharti ya dhamana kwa dhamana iliyokuwa wazi.
“Nimeona kwenye vyombo vya habari leo kwamba wale wabunge waliokuwa wanataka kunisalimia nilipokuwa magereza ni wasaliti wa chama cha CCM.
“Mheshimiwa Rais wengi walinisalimia wakiwemo wachungaji, masheikh, wabunge na viongozi mbalimbali, sidhani kama hatua hii ilikuwa ni usaliti isipokuwa upendo ambao ni muhimu kwa binadamu yeyote pale anapokuwa na matatizo.
“Mheshimiwa Rais nimeogopa sana kwa kauli hii, je Taifa linakwenda wapi? Hivi kweli sisi wabunge ni maadui? Kama viongozi tutafikiri utengano ni moja ya njia ya kuimarisha vyama vyetu, bila shaka tutakuwa tunalitendea Taifa ubaya,” alisema Lema.
Mbunge huyo alisema dhambi hiyo ikikomaa ni wazi kwamba lugha za kidini, ukanda na ukabila hazitaacha kukomaa.
Alisema ni muhimu sasa wakajenga utamaduni wa kuhimiza mshikamano wa kitaifa bila kujali itikadi kama kweli wanapenda masikini na wanyonge.
“Nawaomba wabunge wenzangu walionijali wakati niko gerezani wasijisikie vibaya kwani walifanya jambo jema na muhimu kwa wakati muhimu sana katika maisha yangu ninatarajia kuwa Spika wa Bunge atatoa neon juu ya kauli hii ya Rais.
“Mheshimiwa Rais wakati wa msiba wa Christina Lissu dada yake na Tundu Lissu, nilikuona katika msiba ule wewe na mama yetu mke wako, je wewe ulikuwa unasaliti chama chako?
“Meshimiwa Rais neno la Mungu linasema wapendeni maadui zenu, waombeni wanaowadhi, wabarikini wanaowaonea kwani kufanya hivi ni kuishi kwa thawabu za Mwenyezi Mungu,”alisema Lema.
Mbunge huyo alisema pamoja na hali hiyo ya kuzuiwa lakini aliwashukuru wabunge wa CCM kwa kwenda kumjulia hali, akiwa nyumbani kwake baada ya kutoka gerezani.
“Sina la kusema katika hili kama Rais alikuwa anajua hawakuja kuniona gerezani lakini niwashukuru wabunge wa CCM wote waliokuja kunijulia hali nyumbani. Sisi kama nchi tunatakiwa kuwa na umoja badala ya kuanza kubaguana kwa itikadi zetu za vyama.
“Mdogo wangu wa kike amepata mchumba lakini familia ya huyo mchumba wake inatokana na CCM je tuvunje vikao vya harusi kwa sababu ya tofauti ya vyama?
“Jibu ni hapana sisi ni Watanzania ni lazima tuishi kwa kupenda na kwa umoja kama ambavyo utamaduni wetu unatutaka na si vinginevyo,” alisema.
Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka jana mjini Dodoma nje ya viwanja vya Bunge na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Novemba 4 mwaka jana akikabiliwa na kesi mbili namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.
Katika kesi ya kwanza ya jinai namba 440, anadaiwa kati ya Oktoba 22 mwaka jana maeneo ya Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro, katika mkutano wa hadhara alitoa maneno yenye kuleta tabaka miongoni mwa jamii kwa kutoa matamshi yenye chuki, kuibua nia ovu kwa jamii.
Katika kesi ya pili namba 441, alidaiwa kwamba, Oktoba 23, mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Shule ya Sekondari Baraa, Lema alitoa maneno kuwa:
“Kiburi cha Rais kisipojirekebisha, Rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu, nimeota Mwaka 2020 haitafika Mungu atakuwa ameshamchukua maisha yake,”.
Februari 27, mwaka huu, Mahakama ya Rufaa Tanzania ilifuta rufaa mbili za Jamhuri dhidi ya Lema baada ya mawakili wa Serikali kuieleza mahakama hiyo kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), hana nia ya kuendelea na rufaa, hivyo kuiomba mahakama kuzifuta rufaa hizo zilizokuwa zinahusu dhamana ya mbunge huyo.
Tuesday, March 14, 2017
Sophia Simba afunguka Kujiunga na chama kingine
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Sophia Simba CCM), amevunja ukimya na kusema hana mpango wa kuhamia chama chochote pinzani huku akisema adhabu aliyoipewa na chama hicho ameipokea kwa mikono miwili na hana kinyongo na chama hicho.
Sophia alitoa kauli hiyo Jumatatu katika mahojiano maalumu na Gazeti la MTANZANIA yaliyofanyika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.
“Kwanza una bahati msimamo wangu ni kutozungumza na waandishi wa habari ila kwa kuwa ni wewe haya. Kuhusu adhabu ya chama binafsi nimeipokea kwa mikono miwili na sina kinyongo na uamuzi wa chama changu hata kidogo. Ninajua wapo waliozusha, eti baada ya uamuzi wa Dodoma nimekwenda kukutana na mwanasiasa mmoja wa upinzani, taarifa hizi si za kweli na sitofanya hivyo, nimetoka Dodoma na kurejea hapa nyumbani kwangu Dar es Salaam nimepokewa na watoto wangu, ndugu na marafiki zangu.
Aliongeza “Napenda kuwaeleza Watanzania wote, wafahamu sina mpango wa kujiunga na chama chochote cha upinzani. Na unajua CCM ina makundi mawili, la kwanza ni wanachama wenye kadi na la pili wakereketwa ambao ni wengi nami nitaingia katika kundi hilo na si kuhama,” alisema Sophia.
Wasomi watofautiana kuhusu timua timua ya Ccm
SIKU chache baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwafukuza wanachama wake 12, akiwamo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba, baadhi ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa wametoa maoni tofauti kuhusu hatua hiyo, wengine wakitofautiana nayo na wengine kuiunga mkono.
Machi 11 mwaka huu, mbali na chama hicho kuwafutia uanachama viongozi wake hao, pia kilitoa onyo kali kwa wanachana wengine 12 baada ya Halmashauri Kuu kupokea taarifa ya tathimini ya Uchaguzi Mkuu uliopita.
Mbali na timua timua hiyo, juzi pia Mkutano Mkuu wa chama hicho, uliridhia mapendekezo ya mabadiliko ya wajumbe wa sekretarieti yaliyowasilishwa na Mwenyekiti Rais Dk. John Magufuli, ambayo pia yamemwondoa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai.
Wengine ni Katibu wa Uchumi na Fedha, Zakia Meghji ambaye ameteuliwa kuingia katika kamati ambayo itafanya tathimini ya Uchaguzi Mkuu visiwani Zanzibar na Katibu wa Oganizesheni wa CCM, Muhamed Seif Khatib.
PROFESA MPANGALA
Akitoa maoni yake jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea urais ndani ya CCM, ni makada wengi walijitokeza, lakini kinachoshangaza waliochukuliwa hatua ni wale waliokuwa wakimuunga mkono Edward Lowassa.
Alisema ni haki ya kidemokrasia mwanachama wa CCM kumuunga mkono yule anayeona anafaa, hivyo haikuwa kosa kwa makada hao kumuunga mkono Lowassa katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
“Kinachoonekana waliochukuliwa hatua ni wale waliomuunga mkono Lowassa, sasa ninajiuliza ni kwanini wakawaacha wakati ule? Na waliogombea na kuonyesha upande walikuwa ni wengi mbona hawajaguswa?
“Kwa msingi huu, waliotimuliwa wameonewa… hii si dalili nzuri, inaua demokrasia na si nzuri kwa maendeleo ya chama chenye heshima na chenye uzoefu kama CCM,” alisema Profesa Mpangala.
DK. BANA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema timua timua iliyofanyika ndani ya CCM ni kuwarudisha watu kwenye maadili na kwamba hakuna aliye juu ya chama.
“Kilichofanyika ni kizuri, wale ambao hawana utii lazima wawajibishwe, mfano kina Sophia Simba hawakukubaliana na maamuzi ya Kamati Kuu wakati ule na ilikuwa utovu wa nidhamu… lazima uheshimu maamuzi ya wengi.
“Kwanza ni wanafiki kwa sababu wangekuwa wanampenda kweli Lowassa, wangeonekana siku ile ile nao wangeondoka naye kwenda Chadema,” alisema Dk. Bana.
DEUS KIBAMBA
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema atakuwa kichaa akisema waliotimuliwa wameonewa kwa sababu utaratibu kama huo huwa unafanywa na vyama vyote duniani.
Alisema kinachomshangaza ni CCM kuwatimua makada hao kutokana na kuwa na maoni tofauti kuhusu mgombea ambaye wanamtaka.
“Ingekuwa wamefuja fedha, wameiba mali za chama, wamekichafua chama labda wamelewa, makosa yoyote yanayovuruga chama ningewaunga mkono kwa asilimia 100, lakini kosa lao ni kuwa na maoni tofauti kuhusu mgombea wanayemtaka.
“Imenishangaza sana ingekuwa wamefanya hayo baada ya uteuzi wa chama halafu wakatoka kwenda kumuunga mkono mgombea wa chama kingine, hapo sawa.
“Vyama vya siasa vikiendelea hivi, kwamba wanaokuwa tofauti juu ya wanayempenda, ukiwa na maoni tofauti unafukuzwa, basi hiyo demokrasia itakoma kabisa, kwa sababu hata sasa vyama vyote hakuna demokrasia, hata vya upinzani mtu akitofautiana na mwenyekiti anafukuzwa uanachama,” alisema Kibamba.
Kibamba alisema kilichofanyika Dodoma inaweza kutishia wale waliobaki ndani ya chama, kwamba wataogopa kunyanyua midomo yao kutoa maoni tofauti, jambo ambalo ni hatari.
“Hawa waliofukuzwa uanachama wasifikirie sana kujiunga na vyama vingine, wajiunge kupigania mgombea binafsi, ninawakaribisha waje wajiunge kwenye kampeni ya kupigania mgombea huru,” alisema Kibamba.
MADABIDA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, ambaye ni miongoni mwa waliovuliwa uanachama, alisema kwa ufupi: “Sipo tayari kuzungumzia jambo hilo kwa sasa.”
MSUKUMA
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Geita, Joseph Msukuma, alisema taarifa iliyosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa ametoa siku saba kwa Usalama wa Taifa kuomba radhi si za kweli.
Jumamosi iliyopita, Msukuma, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Adam Malima na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, walikamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutaka kufanya uchochezi na vurugu wakati wa vikao vya chama hicho.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Msukuma alisema sauti inayosikika kwenye mitandao ya kijamii si yake.
“Hiyo sauti si yangu na RPC nimemsikia leo (jana) kwenye redio ameshaomba radhi. Kwaheri,” alisema Msukuma kwa ufupi.
Jana, gazeti moja la kila siku lilimnukuu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa akisema kwamba wabunge hao waliokamatwa baada ya kuhojiwa, iligundulika kuwa hawakuwa na kosa lolote.
Mambosasa alisema kulikuwa na tuhuma kwamba makada hao watatu walikuwa wakigawa fedha kwa wanachama ili kuchochea vurugu katika vikao vya CCM.
“Tumefunga jalada lao baada ya kugundua kinachosemwa ni tofauti na kilichopo na tumewarudishia fedha zao,” alinukuliwa.
Vijana wapewa mbinu mpya na Tundu Lissu
MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amewapa mbinu vijana kwa ajili ya kuishi kwa amani katika Serikali ya Rais Dk. John Magufuli.
Amesema kwamba, ili vijana hao wasisumbuliwe na Serikali iliyoko madarakani, wanatakiwa kujua masuala mbalimbali ya kidunia na pia wasiwe waoga pindi wanapopigania haki katika masuala mbalimbali.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, aliyasema hayo juzi mjini hapa wakati akizungumza kwenye mkutano wa umoja wa wanachama wa chama hicho ambao ni wanafunzi wa vyuo vikuu.
“Sisi kama Chadema, hatutarudi nyuma katika mapambano mpaka tutakapochukua dola mwaka 2020.
“Ili tufikie malengo hayo, lazima vijana msiwe waoga, lazima mjue haki zenu na kupambanua mambo mbalimbali kwa sababu Serikali iliyoko madarakani inalenga kutudhoofisha wapinzani.
“Katika mfumo huu wa vyama vingi, ni vema Serikali ikatambua kuwa Chadema inapoikosoa Serikali, haina maana ya kuwachochea wananchi na badala yake inataka maisha ya wananchi yaboreshwe,” alisema Lissu.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama hicho, Devotha Minja, alisema vijana wengi wasomi wamekuwa wakishindwa kupata ajira kutokana na mfumo mbovu uliopo serikalini.
“Sasa basi, nawaomba vijana msikubali kudanganywa na baadhi ya wanasiasa wasioitakia mema nchi hii na badala yake muendeleze mshikamano bila kukata tamaa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja huo uitwao CHASO, Jafar Ndege, alisema ni vema vijana wakawa chachu ya kuleta maendeleo katika Taifa kwani wanayo fursa kubwa ya kuibua mambo ya maendeleo.
Magufuli amewapasulia jipu wabunge wa CCM
Rais John Magufuli amewapasulia jipu wabunge wa CCM kuwa anamuunga mkono Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hata kama wapo miongoni mwao wanaompinga.
Mbali ya kumkingia kifua Majaliwa, Mwenyekiti huyo wa CCM pia amewaonya wabunge wa chama hicho wanaotoa muda wao wa kuchangia bungeni kwa wapinzani, huku akieleza kukerwa na wabunge wanaofifisha vita dhidi ya dawa za kulevya na mmoja akimtuhumu kutoa siri za chama kwa upinzani.
Rais Magufuli aliyekutana jana na wabunge hao Ikulu ndogo ya Chamwino mjini hapa, pia aliwaambiwa kwamba yeye ndiye aliyeamua kusitisha mikutano ya Bunge kuonyeshwa moja kwa moja katika televisheni.
Kikao hicho cha ndani kimefanyika siku moja baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa CCM mjini hapa na kupitisha mageuzi makubwa ya kikatiba na kanuni kwa chama hicho tawala.
Monday, March 13, 2017
Msukuma afunguka mazito, Ni kuhusu alivyokamtwa na Polisi
JOSEPH Kasheku “Msukuma” Mbunge waa Jimbo Geita Vijijini na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Geita ametoa siku tano za kuombwa na radhi na wanaodaiwa kuwa ni maofisa usalama wa Taifa waliotoa taarifa za uongo dhidi yake na kusababisha akamatwe Mjini Dodoma, anaandika Charles William.
Juzi Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, liliwatia nguvuni Msukuma, Hussein Bashe, Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini na Adam Malima, aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mkuranga kwa madai ya kupanga kufanya vurugu katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika jana.
Wanasiasa hao walikamatwa na kuhojiwa, kabla ya kuachiwa kwa dhamana. Hata hivyo Msukuma amesema hawezi kukaa kimya juu ya suala hilo na kwamba wapo maofisa usalama waliosambaza taarifa juu yake na kusababisha hofu lazima wamuombe radhi.
“Hawa ni wapiga dili, Rais lazima aiangalie upya Idara ya Usalama wa Taifa. Wameniundia mimi zengwe, mpaka nikakamatwa, na nchi ikawa kwenye presha, kama chama kisipozungumza mimi nitaenda kuzungumza na watoto wangu kama Askofu Gwajima (Josephat),” amesema.
Mbunge huyo anayesifika kwa vituko visivyoisha, amesema atapigania heshima yake kwani hajawahi kupata kashfa na lazima atashinda.
“Sitazungumza kitaifa, nitaenda kuzungumza na wapiga kura jimboni kwangu, nieleze kwanini watu wametengeneza kinyago wakakiweka sebuleni halafu kinawatisha wenyewe. Kama kuna usalama wa taifa aliyeshiriki natoa siku tano awe ameniomba msamaha,” amesema Msukuma.
Hofu ya kuibuka kwa vurugu katika mkutano mkuu wa CCM uliofanyika jana iliibuka baada ya juzi Halmashauri Kuu – NEC ya chama hicho kuchukua uamuzi wa kuwafukuza viongozi mbalimbali wanaodaiwa kuwa walikisaliti chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Waliofukuzwa uanachama ni pamoja na wenyeviti wa CCM katika mikoa minne wakiwemo Ramadhani Madabida (Dar es Salaam) na Jesca Msambatavangu (Iringa). Sophia Simba, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum alikutana na kadhia hiyo.
Chanzo: Mwanahalisi
Sunday, March 12, 2017
Moses Machali kayataja Mambo mawili yaliyomfanya ahamie CCM
Leo kwenye mkutano mkuu maalum wa CCM, aliyekuwa mbunge wa Kasulu kwa tiketi ya NCCR kabla ya kuhamia ACT Wazalendo, Moses Machali ametangaza rasmi kuhamia CCM na amezitaja sababu mbili zilizomfanya afanye hivyo ikiwemo utendaji wa Rais Magufuli
Rais Magufuli: Hakuna tena ombaomba CCM
Dodoma. Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk John Magufuli amesema chama hicho hakitambembeleza mtu kukichangia katika shughuli mbalimbali.
Akihutubia mkutano Mkuu wa CCM unaofanyika leo Dodoma, Dk Magufuli amewaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa kwa miaka yote CCM kimekuwa kikiomba hata kwa watu ambao hawastahili.
“Matokeo yake wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kudhalilisha. Hakuna tena omba omba hatutaki kumbembeleza mtu akitaka kutuchangia atuchangie,”amesema.
Amesema kuwa chama hicho kina utajiri unaokiwezesha kujitegemea na kwamba mwanachama atakayetumia mali za chama kwa maslahi binafsi atachukuliwa hatua kali.
Ukumbi mpya wa CCM wapewa jina la Kikwete
Dodoma. Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM wamekubaliana kuita ukumbi mpya uliopo eneo la Dodoma Makulu ‘Kikwete Hall’.
Makubaliano hayo yametokana na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Rais Dk John Magufuli kupendekeza kwa wajumbe hao ukumbi huo uitwe Kikwete.
“Leo tumekaa katika ukumbi huu mzuri kuna watu wamefanya kazi na miongoni mwao atakuwa ni Mzee wetu Jakaya Kikwete (Rais Mstaafu wa awamu ya nne). Mtakumbuka kabla ya hapa tulikuwa tukikaa kule yanatolewa magunia tunakaa,”amesema.
Wajumbe hao walikubaliana na wazo hilo na baadaye Rais Magufuli walishikana mkono na Rais Kikwete.
Wanachama wa Chadema wapigwa, wachaniwa mashati
Dodoma. Mwenyekiti wa Chadema wa Kanda ya Kati, Alphonce Mbasa amesema wanachama wao waliopigwa mjini Dodoma na wafuasi wa CCM, pia wamechaniwa mashati yao.
Akizungumzia tukio la Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Kunti Majala kubebwa mzobemzobe kumnusuru asipate kipigo kutoka kwa wafuasi wa chama hicho, Mbasa amesema watu aliokuwa nao mbunge huyo wamepigwa.
“Ni kweli tukio hilo lipo. Waliopigwa zaidi ni dereva Stephen Masawe na mtumishi wa chama wa kanda, Justin Wiliam ambao kwa sasa taratibu zinafanyika ili wapelekwe hospitali. Lakini mbunge aliokolewa na polisi ingawa alisukumwasukumwa,”amesema Mbasa.
Tukio hilo lilitokea saa 7:00 mchana wakati Kunti na wenzake wawili walipopita mbele ya jengo la makao makuu ya CCM, maarufu kama White House ambamo mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho ulikuwa ukiendelea. Wakati mkutano ukiendelea, gari la Chadema lilipita karibu mara tatu likiwa linapeperusha bendera za chama hicho cha upinzani kabla ya kusimamishwa baada ya kupita karibu zaidi.
Kipigo hicho kilifuatia gari hilo kusimamishwa na watu waliokuwa wamevalia nguo za kijani ambao walizuia barabarani na hivyo kumlazimu dereva kusimama na ndipo walipoanza kupigwa.
Hata hivyo, Mbasa amesema gari hilo lilikuwa limefungwa bendera kubwa mbili ambazo wakati wote hutumika katika magari hayo yaliyoandikwa “M4C” ubavuni na ndiyo sababu likatambulika kwa haraka kuwa ni la Chadema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa amesema hakuwa na taarifa za tukio hilo kwa sababu alikuwa katika msafara wa viongozi na ameahidi kulifuatilia.
Bashe: Sina hofu na timua timua ndani ya CCM
Mbunge wa Nzega Mjini Hussein Bashe amefunga mazito leo asubuhi kuhusiana na sakata la timua timua linaloendelea dhidi ya wanachama wasaliti ndani ya CCM huko Jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM.
Mbunge huyo amesema hawezi kuwa na hofu ya aina yeyote kwa kuwa hana jambo baya alilolifanya ndani ya chama hicho hivyo hawezi kuteteleka na wanaotimuliwa wanachama.
“Sina hofu na timua timua ya wanachama wasaliti kwasababau naamini wamefanya maamuzi kwa kupitia mchakato ndani ya chama, kwa hiyo sina hofu kwasababu chama chetu kinaongozwa na katiba pamoja na kanuni zilizopo unakuwa na hofu pale unahisi kuna jambo umelifanya kinyume na taratibu”-Alisema Bashe
Kwa upande mwingine Mbunge huyo amegoma kuzungumzia sakata la yeye kushikiliwa na Jeshi la Polisi hapo jana na kusema suala hilo kamuachia Katibu Mkuu wa chama hicho ndugu Abdurahaman Kinana.
