Monday, December 19, 2016
Mchungaji alia na waumini sakata la bwana harusi.
Mbeya. Sakata la bwana harusi mtarajiwa kumkimbia bibi harusi kanisani, limemuibua Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Isanga jijini hapa, Andagile Mwakijungu ambaye amewalaumu waumini kusambaza habari za uongo.
Ijumaa iliyopita, bwana harusi huyo aliyetajwa kwa jina la Samuel John hakufika kanisani kufunga ndoa na Given Mgaya katika muda aliotakiwa kufanya hivyo.
Akizungumza wakati wa ibada ya kwanza jana asubuhi, Mchungaji Mwakijungu alisikitishwa na kile alichodai kuwa ni uongo wa waumini waliousambaza kuwa bwana harusi alitoweka baada ya kupigiwa simu kwamba bibi harusi ni mjamzito.
“Waumini acheni kusambaza maneno ambayo hamna uhakika nayo, kwani uongo ni kama mtu muuaji anayeua binadamu mwenzake kwa panga. Tuendelee kutafuta amani na kumtumikia Mungu kwa njia iliyo sahihi,” alisema.
Akifafanua kwa waandishi waliokuwa kanisani hapo, mchungaji huyo alisema hadi sasa hakuna anayefahamu ukweli wa kiini cha bwana harusi huyo kutofika kanisani wakati taratibu zote za awali alishiriki na kushirikishwa.
“Ni kweli Ijumaa ilikuwa ifungwe ndoa, lakini bahati mbaya dakika za mwisho kijana wa kiume hakutokea kanisani na hata nilipompigia simu alinijibu anakuja hadi saa saba mchana ikawa kimya huku bibi harusi akiwa hapa kanisani,” alisema.
Akizungumzia taratibu za ndoa hiyo, mchungaji huyo alisema aliitangaza siku 21 kwa mujibu wa sheria na hapakuwapo na pingamizi lolote.
Alisema kutokana na hali hiyo Alhamisi jioni ikiwa ni siku moja kabla ya ndoa alikutana na kuzungumza na wanandoa hao huku kila mmoja akiwa mwenye furaha na kupeana miadi ya kuwahi ili wamalize shughuli yao mapema.
0 comments:
Post a Comment