Thursday, November 10, 2016
Wabunge wapongezwa
MTANDAO wa Vikundi vya Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA) wamewapongeza wabunge kwa kuangalia kwa kina na kuukataa Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Jumuiya ya Ulaya (EU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EPA).
Mviwata imebainisha kuwa wabunge hao wameangalia zaidi mustakabali wa wakulima wadogo na uchumi wa kitaifa katika suala hilo, kwa kuwa uchambuzi wa EPA ni muhimu kama nchi kwa kuwa ungekubalika ungekuwa na athari mbalimbali kwa taifa na ikiwa ni pamoja na upotevu mkubwa wa mapato ya nchi.
Mratibu wa Mviwata Mkoa wa Manyara, Martine Pius alipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kutosaini makubaliano hayo kwani ni hatua ya muhimu katika kuondoa changamoto zinazoonekana katika makubaliano.
Pius alisema wabunge ambao makubaliano hayo yalipelekwa kwao, wamejadili kwa kina na uamuzi wao umewafurahisha wakulima nchini kwa kuwa yanagusa maendeleo ya wananchi wa Tanzania hasa wakulima wadogo kwa kuwa kama yangepitishwa yalikuwa ni mwisho wa wakulima wadogo.
Alisisitiza kuwa ikiwa kutaondolewa vizuizi vya kibiashara, wakulima wakapata ruzuku na ruzuku za masoko, itawasaidia kuwalinganisha na wakulima wa Jumuiya ya Ulaya.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Sabatho Nyamsenda akizungumza katika ufunguzi wa warsha na Mkutano Mkuu wa Tisa wa Mviwata uliofanyika wilayani Babati jana, alisema uchambuzi wa EPA ni muhimu kama nchi na ndio maana wabunge wakazungumzia na kufanya uchambuzi wa kina kwa kuwa tayari Rais John Magufuli katika uongozi wa awamu ya tano amekwisha onesha njia kuhusu EPA na athari zake.
0 comments:
Post a Comment