Monday, November 7, 2016
HATIMAE SERIKALI IMEKIRI KUWA BANDARINI MIZIGO IMEPUNGUA.
SERIKALI imekiri mizigo inayoingia kwenye bandari ya Dar es Salaam imepungua kwa asilimia 5.47 na kutoa sababu kadhaa, ikiwemo wafanyabiashara kubanwa kulipia kodi, hali iliyofanya kukimbia kutumia bandari hiyo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametaja sababu za kupungua mizigo hiyo kuwa ni pamoja na kudorora kwa bei ya shaba katika soko la dunia, hali inayofanya mizigo inayotoka Zambia kupungua.
Profesa Mbarawa alikuwa akijibu hoja mbalimbali za wabunge walizotoa wakati wakichangia kwenye Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018 na Mwongozo wa Bajeti ya serikali kwa mwaka 2017/2018.
Hata hivyo, Waziri huyo alisema kupungua kwa mizigo si kwa bandari ya Dar es Salaam pekee, bali hata nchi za jirani hali hiyo imewakumba na kutolea mfano kwa bandari ya Mombasa, Kenya ambayo mizigo imepungua kwa asilimia 1.5 na Durban, Afrika Kusini imepungua kwa asilimia 10.
Akizungumzia madai ya wabunge ya uchumi wa nchi umedorora na kitendo cha serikali kuhamishia fedha zake kutoka benki za biashara kwenda Benki Kuu (BoT), Dk Kijaji alisema serikali imeachana na kukuza uchumi wa taifa kwa kutegemea kodi za wafanyakazi pekee.
Badala yake imeamua kuwabana wafanyabiashara walipe kodi ili kukuza uchumi wa taifa sambamba na kodi za wafanyakazi serikalini na waliopo kwenye sekta binafsi.
Kuhusu benki kufilisika kutokana na fedha kuhamishiwa BoT alisema, “benki zetu wavivu, zipo Dar es Salaam pekee na kwenye taasisi za serikali, kwa nini haziwafuati wananchi walipo, serikali imechukua pesa yake kama mteja...tunamkopesha mteja na hatujui pesa inachofanyia, CRDB imepata hasara kwa sababu pesa zao waliozikopesha hawana uwezo wa kuzikusanya na serikali ndio imeshachukua pesa yake”.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akikazia hilo alisema, “uamuzi wa serikali wa kuondoa fedha zake na za taasisi zake za umma kwenye benki za biashara na kuweka BoT utaendelea, hautabadilishwa, tumepigwa sana, benki zilipata faida kwa mgongo wa wanyonge masikini, sasa basi waende vijijini”.
0 comments:
Post a Comment