SHIRIKA la ndege la FastJet limepunguza idadi ya ndege zake kutoka tano zilizokuwepo awali na kubakiwa na ndege mbili tu.
Imedaiwa hatua hiyo imefuatia ujio wa ndege mbili aina ya Bombadier Q400
za serikali zilizokodishwa kwa shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Imeelezwa ujio wa ndege hizo za ATCL umeishtua FastJet hivyo kuona
kwamba haitaweza ushindani kutokana na gharama za uendeshaji wa ndege
zake kuwa kubwa kuliko zile za ATCL.
Meneja wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe (SIA),Hamisi
Amiri,amesema ndege mbili za FastJet zilizopo ndiyo zinazoendelea
kufanya safari nchi nzima, kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani na
nyingine inakwenda nchi jirani za Zambia, Malawi, Zimbabwe na Afrika
Kusini.
“Kinachofanyika sasa ni kuwa hapa Mbeya kulikuwa na ndege mbili za
FastJet kwa siku sasa hivi imebakia ndege moja, hivyo abiria wa ndege
ya asubuhi na jioni wanaunganishwa pamoja na kupandishwa ndege moja”
alisema Amiri.
Amiri alisema awali ndege ya asubuhi ya FastJet, ilikuwa inaondoka
uwanjani hapo saa 3:00asubuhi, lakini kuanzia Ijumaa ya wiki iliyopita
ndiyo tatizo limeanza, ambapo ndege hiyo ilikuwa inaondoka saa
5:00asubuhi, saa 6:00 mchana na siku nyingine saa 7:00 mchana.
Kwa mujibu wa Amiri, ili kuwaunganisha abiria wake FastJet wamekuwa
wanawapigia simu abiria, na wale ambao wanakuwa hawajapatikana, huwa
wanafika uwanjani hapo na kukuta kukiwa hakuna ndege, hali inayoleta
usumbufu kwa abiria.
“Hivi sasa asubihi abiria wanaokuja hapa SIA wanakuwa zaidi ya 250 hadi
300, wote wanataka kusafiri na ndege moja yenye uwezo wa kubeba abiria
150.Wanachofanya FastJet wanatumia ule mtindo wa abiria aliyewahi kufika
uwanjani ndiyo anakuwa wa kwanza kuondoka” alisema Amiri.
Aliongeza hivi sasa abiria wamekuwa wanafika uwanjani hapo kuanzia
saa11:00 alfajiri, hivyo waliowahi ndiyo huwa wanahesabiwa hadi abiria
wa 150, hao ndio wanaoondoka hali inayopelekea asubuhi kunakuwa na
foleni ndefu SIA.
Amiri alisema hivyo hata kama abiria ilikuwa ni siku yake ya kusafiri,
na alikuwa hana taarifa juu ya uwepo wa abiria wengi, anachelewa kufika
uwanjani hapo, na akifika anakutana na foleni ndefu, hivyo anakuwa yupo
nje ya abiria wanaotakiwa kusafiri.
Meneja wa SIA Amiri alisema hali hiyo imekuwa inawachanganya abiria
wengi, ambapo juzi abiria walitaka kuvunja milango uwanjani, wakidai
kama vipi watapigana kwenye ndege ama watadandia mabawa ya ndege, hali
ambayo imekuwa inapelekea usumbufu mkubwa.
Aliongeza hivyo kutoka Ijumaa hadi jana Oktoba 3, mwaka huu hali ilikuwa
mbaya, lakini Oktoba 4, mwaka huu kidogo hali imekuwa nzuri kwani
abiria wote wameweza kusafiri, na inaonyesha wengi wameamua kusafiri kwa
njia nyingine ikiwemo usafiri wa mabasi.
Aliongeza hatua hiyo inatokana na kishindo cha ujio wa ndege mbili za
ATCL, ambapo Fast Jet wamekuta gharama ya kuziendesha ndege zao ni
kubwa, hivyo wamekuta hawataweza kushindana na ATCL hivyo nao wameamua
kuzirudisha ndege zao kubwa ili wanunue ndege ndogo.
Uchunguzi uliofanywa na Muungwana blog wanjani hapo,unaonyesha FastJet
walikuwa wanafikiri serikali haitaweza kununua ndege mbili kama
ilivyokuwa imeahidi, hali inayoonyesha walikuwa hawajajipanga vizuri.
0 comments:
Post a Comment