Tuesday, November 15, 2016
Wakulima Tunduru wapata soko la korosho
WAKULIMA wa korosho Wilaya ya Tunduru, wameondokana na umasikini kutokana na kupata soko la uhakika baada ya Kampuni ya Namela General Trade kushinda zabuni ya kununua zao hilo wakulima kwa bei ya Sh 3,757 kwa kilo, ikizishinda kampuni nyingine saba.
Hadi kufikia Novemba 14, kulikuwa na zaidi ya tani 541 zilizoingizwa katika ghala la Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru (Tancu) ambako kampuni hiyo ilipewa kununua korosho tani 400 huku Kampuni ya Machinga iliyoshinda nafasi ya pili katika mnada huo, ikipata kibali cha kununua tani 141 kwa bei ya Sh 3,750.
Juzi, Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma, iliingia katika historia mpya tangu ianzishwe mwaka 1905, kwa wakulima kuuza zao hilo kwa njia ya mnada, jambo liliwafurahisha wakulima na wananch wengine.
Kampuni zilizoomba kununua korosho kwa njia ya mnada wilayani Tunduru zilikuwa saba, Namela iliomba kununua tani 400,000 kwa bei ya Sh 3,757, Machinga tani 400,000 kwa bei ya Sh 3,750, ETC Ltd ilitangaza bei ya Sh 3,700, Vikat Ltd 250,000 kwa bei ya Sh 3,277, Maviga East Africa tani 400 kwa Sh 3,500, na kampuni nyingine mbili ambazo ziliomba kununua kwa bei ya chini.
Akizindua mnada huo uliofanyika katika viwanja vya Tancu, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera amewataka wananchi wa Tunduru kuwa na imani na serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi ambayo imeonesha dhamira ya dhati kuwakomboa wananchi na maadui watatu ambao ni umaskini, ujinga na maradhi.
Homera amewataka kuendelea kuiunga mkono serikali wakati huu ambao imejipanga kuhakikisha inaondoa vitendo vya dhuluma, wizi na mambo mabaya ambayo kwa muda mrefu yamekuwa kero kwa Watanzania.
Aidha, amewakumbusha wakulima wa korosho kujiwekea akiba na kutumia fedha hizo katika mambo ya msingi, badala ya kuzielekeza katika anasa, jambo linaloweza kuwarudisha nyuma. Ametoa siku tatu kwa kampuni zilizoshinda kuanza malipo ili wakulima ajiandae na msimu mpya wa kilimo mashambani.
Meneja Mkuu wa Tancu, Iman Kalembo alisema kazi ya kukusanya korosho kutoka katika vyama vya msingi vya ushirika ilianza tangu Septemba, lakini walishindwa kuanza mnada mapema kutokana na changamoto mbalimbali kama vile uhaba wa magari ya kubeba zao hilo kutoka shambani hadi kwenye maghala




0 comments:
Post a Comment