Propela

aa

million ads

Millionaire  Ads

Tuesday, November 15, 2016

Nyota wa majaribio wamvutia kocha Azam

KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Zeben Hernandez, ameweka wazi kuwa amefurahishwa na viwango vya baadhi ya nyota waliokuja kufanya majaribio ya kujiunga na timu hiyo kwenye usajili wa dirisha dogo ulioanza leo. Azam FC imemaliza programu ya kukifanyia tathimini kikosi chake kwa kuichapa Ruvu Shooting mabao 3-1 kwenye mchezo wa kujipima ubavu uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi. Wachezaji tisa waliopimwa ni pamoja na mabeki wa kati Nkot Mandeng Eric (Coton Sport De Garoua, Cameroon), Kone Nabil Ibrahim (Asec Mimosa, Ivory Coast). Wengine ni kiungo mkabaji Kingue Mpondo Stephane (Coton Sport Garoua, Cameroon), Abdallah Khamis pamoja na washambuliaji Yaya Anaba Joel (Coton Sport Garoua, Cameroon), Samuel Afful (Sekondi Hasaacas, Ghana), Bernard Ofori (Medeama, Ghana), Konan Oussou (Tala’ea El-Gaish SC, Misri) na Jean Karekezi. Mabao mawili kati ya matatu ya Azam FC yalifungwa na nyota waliokuwa majaribio, ambao ni Ofori aliyefunga la kwanza kwa kichwa akimalizia krosi safi ya Gadiel Michael na Afful akitumia juhudi binafsi kwa kumzidi maarifa beki pembeni ya uwanja na kupiga shuti kali lililojaa wavuni. Hernandez alisema kuanzia sasa anatarajia kupeleka mapendekezo yake kwa uongozi wa timu hiyo juu ya nyota gani kati ya hao wasajiliwe, huku akisisitiza kuwa wachezaji watakaosajiliwa wataisaidia Azam FC. “Raundi ya kwanza imemalizika na tumeona mapungufu ambayo tunataka kuyarekebisha kwa ajili ya raundi ya pili na ndio maana tumejaribu kutafuta wachezaji ambao tunahisi wanaweza kutusaidia kwenye timu raundi ya pili na michuano mingine,“ alisema kocha huyo. Kocha huyo wa zamani wa Stanta Ursula ya Hispania, alisema anaamini ya kuwa kikosi chake kikiingia raundi ya pili kitaweza kupambana ipasavyo na kupata matokeo mazuri. Mara baada ya mchezo huo wa juzi dhidi ya Ruvu Shooting, benchi la ufundi la Azam FC limewapa mapumziko ya wiki mbili wachezaji wa kikosi hicho kabla ya kuanza tena mazoezi Desemba 3 mwaka huu kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na michuano ya Kimataifa.

0 comments:

Post a Comment