Propela

aa

million ads

Millionaire  Ads
Showing posts with label AJALI. Show all posts
Showing posts with label AJALI. Show all posts

Wednesday, February 15, 2017

Taarifa ya Mgodi mwingine kufukia watu Mara

Taarifa kutoka Butiama kwenye Mkoa wa Mara leo ni kuhusu miili ya watu wawili kupatikana February 14 2017 kwenye Mgodi wa Buhemba ambapo kwa taarifa za awali watu 13 wameokolewa wakiwa wamejeruhiwa baada ya kufukiwa ndani ya mgodi. Kutoka kwenye eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Butiama Annarose Nyamubi amesema “Ni kweli kabisa kwenye Wilaya ya Butiama Magunga ulipo mgodi wa zamani wa dhahabu wa Buhemba shimo moja limefukiwa na kifusi saa 3 asubuhi” “Mpaka saa 7 mchana tuliweza kuokoa watu 13 na wengine wanaendelea na matibabu huku wengine wakiwa wameruhusiwa wako nyumbani, kuna Wachimbaji wengine wanne bado wanatafutwa na idadi inaweza kuongezeka” “Idadi inaweza kuongezeka kwasababu kuna Wachimbaji ambao huwa wanazamia bila kujisajili majina yao kabla ya kuingia mgodini, wale ambao huwa wanajisajili ndio rahisi kutambua rekodi zao… tunavyoendelea na zoezi” – DC Annarose

Tuesday, January 31, 2017

Muuguzi hospitali ya Wilaya afa akichota maji

Muuguzi hospitali ya Wilaya afa akichota maji Tuesday, January 31, 2017 MUUGUZI wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Magreth Anatoly (57), amefariki dunia kwa shinikizo la damu wakati alipokuwa akisomba maji kutoka kwenye tangi la lori lililokuwa limepeleka maji katika hospitali hiyo, ambayo imekumbwa na ukosefu mkubwa wa maji. Mfanyabiashara na kada wa CCM, Peter Zakaria amejitolea kutoa lori lake lenye tangi la maji kupeleka maji katika hospitali hiyo pamoja na Magereza wilayani hapa. Mganga Mkuu wa hospitali hiyo ya wilaya, Calvin Mwasha amethibitisha kufariki kwa muuguzi Magreth, na kueleza kuwa alifariki Alhamisi mchana wakati muuguzi huyo akiwa na wenzake, walipokuwa wakisaidia kazi ya kusomba maji kwa kutumia ndoo kutoka kwenye tangi la lori, lililokuwa limepeleka maji ya matumizi hospitalini hapo. “Muuguzi huyo alipofikisha ndoo aliyokuwa amebeba alikaa kwenye kiti kupumzika na kujisikia hali yake kuwa mbaya na kudondoka chini na kusaidiwa na wenzake waliokuwa naye, lakini alipoteza maisha. Kifo chake kimetokana na shinikizo la damu. Tumepata pigo kubwa kwa mama yetu Anatoly kwani alikuwa kiungo kikubwa kwetu hususani vijana wanaoanza kazi,” alieleza daktari wa wilaya. Muuguzi huyo alizikwa mjini Tarime jana.

Watu 6 wahofiwa kufa Ziwa Tanganyika

WATU sita wanahofiwa kufa maji na shehena ya mizigo yenye bidhaa mbalimbali inasadikiwa kuzama ndani ya ziwa Tanganyika baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupotea kwa zaidi ya siku 10 sasa. Tetesi za kupotea kwa boti hiyo zimezagaa sehemu mbalimbali mkoani Kigoma na Polisi mkoani Kigoma imethibitisha ajali hiyo na juhudi za kuitafuta zinaendelea. Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui alisema boti hiyo iliondoka Januari 21, mwaka huu katika bandari ya Kibirizi kwenda Kalemie katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na hadi leo haijafika ilipokuwa ikielekea. Kamanda Mtui alisema boti hiyo ijulikanayo kwa jina la Mv.Ngendo ya Buchuma, mali ya Mussa Hamisi ambaye ni mkazi wa Ujiji mjini Kigoma, ilikuwa imebeba shehena ya vitunguu na ngano ambavyo vilikuwa vikipelekwa Kalemie ikiwa na watu sita wakiwemo wafanyakazi wa boti hiyo. Kwa mara ya mwisho, Kamanda Mtui alisema boti hiyo ilionekana upande wa DRC na kwamba hadi sasa haijulikana boti hiyo imekumbwa na nini na iko wapi. “Kwa sasa polisi wanamaji kwa kushirikiana na chama cha wamiliki wa maboti Mkoa wa Kigoma tunaendelea na msako wa boti hiyo sambamba na kutoa taarifa kwa mamlaka za Mji wa Kalemie nchini DRC kuhusiana na kupotea kwa boti,” alieleza Kamanda Mtui.

Mvua yaezua paa za madarasa sita na choo

PAA za madarasa sita ya Shule ya Sekondari Kisumwa iliyopo katika Tarafa ya Suba mkoani Mara pamoja na nyumba za walimu na choo, zimeezuliwa na mvua kubwa iliyoambatana na upepo. Mvua hiyo iliyonyesha mwishoni mwa wiki, pia imeharibu nyumba na mazao ya wakazi wa vijiji vya Kisumwa na Mara Sibora mkoani Mara. Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Charles Chacha, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo. Chacha alisema mvua hiyo ilinyesha wilayani Rorya ikiwa ni baada ya zaidi za mwezi mzima ikikumbwa na ukame. Alisema mvua hiyo iliyokuwa imeambatana na upepo mkali, iliezua paa za madarasa sita, nyumba ya mwalimu na choo katika Shule ya Sekondari Kisumwa. Kadhalika, Chacha alisema mvua hiyo pia iliharibu mazao na baadhi ya nyumba za wakazi wa vijiji vya Kisumwa na Mara Sibora. Alisema Kamati ya Maafa chini ya Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Saimon Chacha, itafanya tathmini ya mali iliyoharibika katika shule hiyo na kwa wakazi wa vijiji hivyo. Aidha, Mkurugenzi huyo amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Rorya kuzitumia mvua zinazoendelea kunyesha kupanda mazao yanayokomaa kwa muda mfupi na yanayovumilia ukame.

Thursday, January 19, 2017

AJALI : Basi la Taqwa, Fuso na Lori la mizigo, Watu 5 wafariki Dunia

Ajali mbaya imetokea maeneo ya mswiswi Mbeya ajali imehusisha magari 3 moja Basi kampuni ya Taqwa ikitokea Dar kuelekea na Fuso lilikuwa limebeba ndizi ikitokea Mbeya. Chanzo cha Ajari ni Fuso ilikuwa ina Overtake lori Mara Basi nayo ilikuwa imeshafika ndipo Ajari ilipotokea Dereva wa basi alifariki dunia pamoja na dereva wa fuso na tingo wake majeruhi walipelekwa Hospital lakini mpaka Sasa Hospital wamefariki watu wawili mwanamke mmoja na mwanaume mmoja wote raia wa kongo. M/mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi AMIN

Thursday, January 12, 2017

Aliyenusurika ajali boti arukwa akili

MMOJA wa manusura 33 wa ajali ya boti iliyozama Bahari ya Hindi na kusababisha vifo vya watu 13, amebainika kurukwa na akili na matabibu wa Hospitali ya Rufaa ya Tanga wanaomtibu. Image Juzi Alfajiri, boti ya Burudan, maarufu Sayari, yenye namba za usajili MV 25512, mali ya Suleiman Vuai, mkazi wa Pemba, ilizama karibu na Kisiwa cha Jambe ilipokuwa inatoka bandari bubu ya Sahare jijini Tanga kwenda Pemba ikiwa na shehena ya chakula, bia na abiria zaidi ya 40. Katika ajali hiyo, watoto sita walikuwa miongoni mwa watu 12 waliopoteza maisha huku 33 wakiokolewa na wavuvi wakiwa hai na kukimbizwa kwenye hospitali hiyo, maarufu Bombo. Hata hivyo, jana jioni Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Goodluck Mbwilo, aliambia Nipashe jijini humu kuwa majira ya saa 10 alasiri walipokea maiti ya mtoto mwenye umri kati ya miaka mitano na sita ikiwa imeharibika. Hadi jana saa 9:38 alasiri, manusura 32 walikuwa wameruhusiwa kuondoka hospitalini hapo huku msichana mmoja mwenye umri wa miaka 12 akishindwa kuruhusiwa kutokana na kurukwa akili. Msichana huyo (jina tunalihifadhi) amebainika kurukwa na akili kutokana na ajali hiyo ambacho taarifa za awali zinadai ni mawimbi makali yaliyopiga boti hiyo na kusababisha maji kuingia ndani.

Friday, January 6, 2017

Ajali yaua watu kisumu

Ajali za barabarani zimekithiri, Watu 11 wapoteza maisha katika ajali ya barabarani Kisumu, nchini Kenya. Watu 11 wamepoteza baada ya kutokea kwa ajali ya barabara katika Kaunti ya Kisumu Magharibi mwa Kenya. Ajali za barabarni zimekithiri katika nchi za Afrika hasa afrika ya Mashariki Kamishena wa Kaunti ya Kisumu, Mohammed Maalim amesema chanzo cha ajali hiyo ilikuwa ni mwendo wa kasi wa gari la abiria maarufu kama Matatu ambalo pia lilikuwa limejaa kupita kiasi. Ripoti zinasema kuwa, gari hilo la abiria lilikuwa linatoka katika mji wa Sirare karibu na mpaka wa Tanzania kwenda mjini Kisumu likiwa na idadi kubwa ya abiria. Inaarifiwa kuwa gari hilo liliondoka barabarani na kuanguka shimoni katika eneo la Nyakatch, asubuhi ya leo. Serikali ya Kaunti hiyo inasema inachunguza ni kwanini gari hilo lilikuwa na abiria wengi. Ajali nyingine kama hii ilitokea jijini Kampala nchini Uganda Jumatano wiki hii na kusababisha vifo vya watu 14

Friday, December 16, 2016

Watano wahofiwa kufa maji Ziwa Victoria

Muleba: Watu watano wanahofiwa kufa maji baada ya boti walilokuwa wakisafiria kupinduka jirani na Kisiwa cha Mazinga kwenye Ziwa Victoria. Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Richard Ruyango alisema boti hilo lilizama jana. Alisema uongozi wa wilaya umetoa mafuta kwa ajili ya boti ili kwenda kutafuta miili ya watu hao. Aliwaomba wananchi na hasa wavuvi kutoa ushirikiano kuhakikisha inapatikana. Source: Mwananchi

Saturday, December 10, 2016

Katika kuadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Disemba, 2016 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:- (i) Wafungwa wote wamepunguziwa moja ya sita (1/6) ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2 (i-xx). (ii)Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI, KIFUA KIKUU (TB) na SARATANI (CANCER) ambao wako kwenye “terminal stage”. Wafungwa ambao wamethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya. (iii)Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi ambao umri huo umethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya. (iv)Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya. (v)Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili (Physical disability and mental disability) ambao ulemavu huo umethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya. 2.Aidha, Msamaha huu wa Mheshimiwa Rais hautawahusu wafungwa wafuatao:- (i)Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa. (ii)Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani. (iii)Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani. (iv)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bhangi n.k. (v)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji, upokeaji au utoaji rushwa. (vi)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo (robbery with violence, armed robbery and attempt robbery). (vii)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali (firearms, ammunitions and explosives). (viii)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti, au kujaribu kutenda makosa hayo. (ix)Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane (18) na kuendelea. (x)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo. (xi)Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No. 6/2002). (xii)Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao. (xiii)Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Mheshimiwa Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki. (xiv)Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo. (xv)Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu (Human Trafficking). (xvi)Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu. (xvii)Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji wa nyara za Serikali na ujangili (Poachers). (xviii)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali. (xix)Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali. (xx)Wafungwa walioingia gerezani baada ya tarehe 9/10/2016. 3.Wafungwa wapatao 5,678 watafaidika na msamaha huu baada ya kupunguziwa 1/6 ya vifungo vyao ambapo 1,340 wataachiliwa huru na wafungwa 4,338 watanufaika na kubaki gerezani wakitumikia sehemu ya kifungo kilichobaki. Ni mategemeo ya Serikali kwamba watakaoachiliwa huru watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani. Imesainiwa na; Meja Jenerali Projest Rwegasira KATIBU MKUU WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI 9/12/2016

Bweni la wasichana wa shule ya sekondari ya Mtwara ufundi iliyoko katika Manispaa ya Mtwara Mikindani limeteketea kwa moto leo majira ya saa moja asubuhi. Akizungumza katika eneo la tukio kamanda polisi Mkoani hapa Thobias Sedoyeka amesema kwamba majira ya saa moja katika shule ya sekondari ufundi kulitokea moto ambao ulianza kuwaka katika mabweni ya wasichana ambapo mpaka sasa chanzo hakijajulikana na kuongeza kuwa hakuna madhara yoyote yaliyotokea kwa binadamu na makadirio ya hasara ya thamani ya jengo na mali zilikuwemo bado haijajulikana. Naye mwalimu wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Nanyalika amesema kwamba alikuwepo eneo la tukio wakati bweni hilo la wasichana wa shule ya sekondari ya ufundi linaanza kuteketea ambapo kwa upande wake hajui chanzo cha moto huo hali ambayo imepelekea walimu ambao wanaishi ndani ya shule hiyo kuwa na hali ya sintofahamu kwa kuhofia usalama wao. kwa upande wake mwalimu wa shule ya sekondari Sululu Sekondari iliyoko Mjini Masasi ambae yupo shuleni hapo kwa ajili ya kusahihisha mitihani ya kidato cha pili na alikuwa akitumia moja ya chumba cha bweni hilo amesema kwamba kipindi ambacho wapo katika maeneo yao ya kazi ndipo walipoona moshi unatokea kwenye bweni. Naye mwalimu Masele Francis kutokea shule ya sekondari ya Namwombe iliyoko katika Halmashauri ya Masasi ameeleza kuwa kipindi ambacho anatoka bwenini aliona moshi mkubwa hali ambayo ilimpelekea kurudi ndani ili kuwapa wenzake taarifa. Aidha Afisa Habari wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Bi.Jamad Omary amewatoa hofu walimu pamoja na wanafunzi wa shule hiyo na kuwaomba kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu mbali na hayo amewataka wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani kuwa na ushirikiano wa kutosha pindi kunapotokea tatizo kama hilo na si kuishia kutoa lawama. Hata hivyo Kamanda amesema kwamba taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo ikiwemo chanzo cha moto huo itatolewa baada ya taratibu zote kukamilika.

Wednesday, November 30, 2016

Ajali ya Gari Yaua Watu 6 rukwa

Watu sita wakiwamo mfungwa na wanafunzi wamekufa huku wengine wanane wakijeruhiwa, baadhi yao vibaya baada ya gari dogo walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka mara nne katika Kijiji cha Kipande wilayani Nkasi katika Mkoa wa Rukwa katika barabara kuu ya Mpanda – Sumbawanga. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema ajali hiyo ilitokea saa 8.10 jana mchana katika Kijiji cha Kipande. Aliwataja waliokufa kuwa ni mfungwa wa Gereza la Kitete lililopo Nkasi, Gaudensi Nyambo (27), Gasper Malimi (18) na Kenzi Mwambige (18) wote wakiwa wanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Nkasi na Ofisa Mipango wa Wilaya ya Nkasi, Godfrey Mwanansao. Alisema marehemu wawili hawajatambuliwa huku miili yote ikiwa imehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Rukwa ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga . “Mfungwa Nyambo alikuwa akitumikia kifungo katika Gereza la Kitete wilayani Nkasi ambako alikuwa na kesi nyingine mahakamani alikufa wakati akitibiwa hospitalini hapa,” alieleza Kamanda Kyando. Alisema ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Hiace Nissan Vannette lenye namba za usajili T 966 DHP lililokuwa likiendeshwa na Lusanjo Mwaipopo aliyekimbia baada ya ajali hiyo. Alisema gari hilo lilikuwa likitokea wilayani Nkasi kwenda mjini Sumbawanga ambapo liliacha njia na kupinduka mara nne kabla halijaanguka ndani ya gema. Alisema chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika huku uchunguzi wa kipolisi ukiendelea. Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa, Dk John Lawi alisema majeruhi tisa wamepokewa hospitalini hapo ambao mmoja ambaye ni mfungwa alikufa OPD. Aliwataja majeruhi kuwa ni pamoja na askari Magereza wa Gereza la Kitete, Fortunatus Saanane (44) aliyelazwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU) huku hali yake ikiwa tete. Wengine ni askari Magereza, Francis Elay (30) ambaye alitibiwa na kuruhusiwa. Kwa mujibu wa Dk Lawi, majeruhi wengine ni Mbagala Hale, Mamadelwa Kafadhila, Mathias Mwandaliwa (28) na wengine ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja. Alisema hali za majeruhi hao ni mbaya.