Sunday, February 12, 2017
Bosi wa waganga awauma sikio wananchi
Magu. Kiongozi wa waganga wa tiba asili wilayani Magu ameibuka na kuwataka wananchi kuwaumbua hadharani waganga wanaopiga ramli ili washughulikiwe.
Boniface Kanyerere ambaye ni mwenyekiti wa watalaamu hao wa tiba asili amewaambia wananchi katika mkutano wa hadhara ulioitishwa mjini Magu kuwa, hawana haja ya kuhofia, bali kutoa taarifa haraka ili wahusika washughulikiwe.
Kanyerere amesema wapo baadhi ya waganga ambao huitumia jamii kufanya mambo yao mabaya kwa kuwa haiwaumbui hadharani.
Amesema ramli zinazopigwa kimyakimya ni hatari na zinasababisha wananchi kuhasimiana na kuchochea uvunjifu wa amani miongoni mwa jamii.
“Tukumbuke kuwa kazi ya mganga wa asili ni kutoa tiba kwa mgonjwa anayetaka kutibiwa na siyo kumhamasisha akafanye mauaji au kuzusha hali ya taharuki kwenye eneo lake,” amesema Kanyerere.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Shije wilayani Magu, Alfred Msongambele amesema iwapo kuna mganga wa aina hiyo asiachwe aendelee kutamba wilayani humo, bali achukuliwe hatua haraka.
Msongambele amesema Watanzania wanahitaji utulivu na Amani vitawale ili waweze kufanya shughuli zao za maendeleo na siyo kugombanishwa.



0 comments:
Post a Comment