Propela

aa

million ads

Millionaire  Ads

Thursday, December 8, 2016

Tanzania ina nguvu kazi isiyo na ujuzi

OFISI ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, imesema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara, inakabiliwa na tatizo la kuwa na idadi kubwa ya nguvu kazi yenye kiwango cha chini cha ujuzi ikilinganishwa na mahitaji ya ujuzi katika soko la ajira. Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde, amesema hayo katika hotuba ya uzinduzi wa mafunzo ya stadi za kushona nguo kwa teknolojia za kisasa, kwa vijana 200 kati ya 1,000 waliosajiliwa kushiriki mafunzo hayo katika kiwanda cha Mazava Fabrics & Production Ltd cha mjini Morogoro. Mavunde amesema hali hiyo imeonekana kupitia utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2014 ambao ulionesha kuwa asilimia 79.9 ya nguvu kazi ina ujuzi wa kiwango cha chini, hivyo juhudi za makusudi za kuwezesha upatikanaji wa ujuzi sahihi miongoni mwa nguvu kazi zinahitajika. Amesema, serikali kwa kutambua umuhimu wa kuendeleza nguvu kazi ya taifa, imeandaa programu ya kukuza ujuzi nchini, hususani kwa nguvu kazi iliyo katika soko la ajira kupitia mafunzo maeneo ya kazi. Mavunde amesema, mafunzo hayo yanayofanyika katika kiwanda cha Mazava ni mojawapo ya utekelezaji wa programu ya miaka mitano ya kukuza ujuzi nchini na Julai mwaka huu yalianza katika kiwanda cha TOOKU kilichopo eneo la Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Viwanda (EPZA), Dar es Salaam ambapo vijana wapatao 2,000 wameanza kunufaika na mafunzo hayo kwa awamu. Mkurugenzi wa Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Ally Msaki amesema, katika programu hiyo ambayo ni ya miaka mitano, vijana wapatao 27,000 wanatarajia kunufaika kwa kupatiwa mafunzo ya stadi za ujuzi mbalimbali kwa kuingi mikataba ya wenye viwanda vinavyojihusisha na kazi hizo. Hata hivyo katika kiwanda cha Mazava, serikali imeingia mkataba wa mwaka mmoja kufundisha vijana 1,000 ambao wamesajiliwa baada ya mchujo wa jumla ya vijana 2,030 waliokuwa wameomba kutoka mikoa mbalimbali nchini, na awamu ya kwanza imeanza Desemba mosi mwaka huu kwa vijana 200. Meneja wa Mazava, Nelson Mchukya amesema ni kitu cha ajabu kuona Serikali inawagharamia watu wake kupata mafunzo ya stadi za ujuzi, hivyo aliwataka vijana waliotapa fursa hiyo kuitumia kujifunza kwa bidiii na kuonesha uaminifu kwa serikali yao.

0 comments:

Post a Comment