Sunday, December 4, 2016
Simba wajadili ligi, mkutano mkuu
VIONGOZI wa Matawi wa klabu ya Simba jana wamefanya mkutano na kujadili mwenendo wa timu yao katika Ligi Kuu na Mkutano Mkuu wa dharura utakaofanyika Jumapili ijayo.
Kwenye mkutano huo ulifanyika Makao Makuu ya klabu hiyo yaliyopo mtaa wa Msimbazi Kariakoo na kuhudhuriwa na wanachama 200 kutoka matawi 68.
Awali, akizungumza baada ya kufungua mkutano huo, Rais wa Simba, Evans Aveva alisema mkutano huo utajadili ajenda mbili, ambazo ni mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Mkutano Mkuu wa Dharura utakaofanyika Desemba 11.
“Ndugu viongozi wenzangu nimewaita hapa ili tujadili Mkutano Mkuu unaotarajia kufanyika Desemba 11 na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, hivyo kabla ya kuanza kujadili naomba waandishi wa habari watupishe ili tuweze kuendelea na mkutano wetu, “alisema Aveva huku akishangiliwa kwa makofi.
Mkutano huo ambao ulianza saa tisa alasiri uliohudhuriwa pia na Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Katibu Mkuu, Patrick Kahemele na wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
Awali Rais wa Simba, Evans Aveva alisema Kamati ya Utendaji imeitisha Mkutano Mkuu wa dharura unatarajiwa kufanyika Desemba 11, kwenye ukumbi wa Polisi Osyterbay Dar es Salaam.
Hatahivyo, Baraza la Bodi ya Wadhamini wa klabu hiyo chini ya Katibu wake Mkuu, Mzee Hamis Klimoni juzi lidai kutoutambua mkutano huo na kumuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuuzuia kufanyika.



0 comments:
Post a Comment