Saturday, December 10, 2016
Serikali yaridhishwa usafiri mizigo Dar – Rwanda
SERIKALI imesema mabadiliko makubwa yameanza kuonekana katika usafirishaji wa mizigo ya Rwanda inayopitia nchini, hususan bandari ya Dar es Salaam. Aidha, imeelezwa kuwa, mpaka sasa asilimia 70 ya mizigo yote ya Rwanda inapitia Tanzania.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Rwanda, Francois Kanimba baada ya kutembelea bandari ya Dar es Salaam.
Kanimba akiwa na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Rwanda walikutana katika mkutano wa siku mbili ulioanza juzi wenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kuondolewa kwa vikwazo vya kufanya biashara.
Mwijage alisema biashara kati ya nchi na nchi za Afrika ni ndogo, hivyo ni lazima kujadiliana kwa kina ili biashara ifanyike vizuri.
“Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili ifanyike vizuri, japo zilikuwepo changamoto kadha wa kadha za vikwazo vya biashara zitaondolewa na hatimaye taratibu zote zitakuwa zikifanyika vizuri,” alisema Mwijage.
Alisema Tanzania imekuwa ya 180 kati ya nchi 189 katika kuwa na mazingira mazuri ya biashara na hatua hiyo imefikiwa kutokana na kuwepo kwa kusimama mara nyingi kwenye maeneo ya mipakani, kuchelewa kwa mizigo katika mizani na hata ukaguzi kucheleweshwa bandarini.
Alisema vikwazo kama hivyo kwa pamoja ndivyo vinavyochangia mazingira ya biashara kutokuwa mazuri, jambo ambalo linapigwa vita ili kuondolewa kwa vikwazo vyote ambavyo vitasababisha ufanyaji biashara kutokuwa mzuri.
Hata hivyo, alisema serikali ina mpango utakaohakikisha taasisi zote za ukaguzi wa bidhaa zinazoingia ama kutoka nchini kuwa katika eneo moja ili kuondoa kabisa kero na usumbufu kwa wafanyabiashara.
Waziri Kanimba alisema ipo haja kubwa ya kuwa na muundo wa taaaisi za kiuchumi ambao utaimarisha biashara baina ya nchi hizo na kuhakikisha inafungua milango ya biashara baina ya nchi hizo.
Kuhusu kupotea kwa mizigo ya Rwanda bandarini, alikiri kuwepo kwa mabadiliko katika usafirishaji wa mizigo ya Rwanda na kwamba hali imekuwa nzuri na kuahidi nchi hiyo itaendelea kuitumia bandari ya Dar es Salaam katika shughuli za usafirishaji




0 comments:
Post a Comment