Sunday, December 4, 2016
Ndalichako: Mliosoma pamoja shikamaneni
WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amewashauri wanafunzi waliomaliza katika shule zao miaka ya nyuma kuendelea kudumisha umoja, mshikamano ikiwemo kusaidia namna ya kutatua changamoto zinazozikabili shule hizo.
Alitoa mwito huo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa Wanaujiji waliosoma Sekondari ya Ujiji iliyopo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma. Akiwa mgeni rasmi katika mkutano huo, alizindua pia mfuko wa kuwezeshana wana umoja huo.
Alisema, wazo lililobuniwa na Wanaujiji hao linafaa kuigwa na wanafunzi wengine katika shule mbalimbali hapa nchini kwani kupitia umoja huo ni rahisi kusaidia kutatua baadhi ya changamoto zinazozikabili shule walizosoma.
“Mbali na hayo ndugu zangu, yafaa sana kuendelea kudumisha amani, umoja, mshikamano na upendo ikiwemo kufanya kazi kwa bidii ili kwa pamoja tuweze kujikomboa kiuchumi. “Nimeguswa sana na umoja wenu huu ambao ni mfano wa kuigwa katika taifa letu, tunahitaji watu wenye mawazo chanya kama ninyi ili kuliwezesha taifa letu kuondokana na watu wanaolalamika kila siku kuwa hamna ajira, tujifunze kupitia umoja wa Wanaujiji waliosoma Ujiji Sekondari,” alisema.
Aidha, Profesa Ndalichako aliwaahidi wana Ujiji hao kuwa, wakati wowote yuko tayari kuwasaidia pale wanapohitaji msaada ili kuhakikisha lengo lao la kuboresha shule yao linatimia.
Awali, Katibu wa wana umoja hao, Seba Mtale alisema, mafaniko ya umoja huo yanatokana na mshikamano walionao wanachama ambapo wamedhamiria kufanya mabadiliko katika shule yao na hata kuinuana wenyewe kwa wenyewe katika umoja.



0 comments:
Post a Comment