Tuesday, December 6, 2016
kajiji chakosa mganga miaka kumi kikihudumiwa na muuguzi asiye na sifa
WANANCHI wa Kijiji cha Mafyeko, wilayani Chunya, wamelalamikia zahanati ya kijiji chao kutokuwa na mganga kwa zaidi ya miaka 10, huku huduma za afya kwenye zahanati hiyo zikitolewa na muuguzi asiyekuwa na sifa ya udaktari.
Malalamiko ya wananchi hao, yalitolewa juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Biti Manyanga, wilayani Chunya mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla.
Mkazi wa kijiji hicho, James Mwakyele, alisema zaidi ya miaka 10, zahanati yao haina mganga na malalamiko yao walifikisha kwenye ngazi husika ikiwamo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya, bila mafanikio.
Alisema, huduma za afya kwenye zahanati hiyo, zinatolewa na muuguzi anayedaiwa kutokuwa kazini muda wote kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya kiafya.
“Kutokana na kukosekana kwa mganga, huku muuguzi wetu naye akisumbuliwa na maradhi ambayo yanamfanya asiwepo kutoa huduma wakati wote, wananchi tunalazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya kwenye zahanati za vijiji vya jirani, hivyo tunaomba utusaidie kumaliza kero hii,” alisema.
Akizungumzia kero hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Sophia Kumbuli, alikiri kuwapo kwa tatizo la ukosefu wa mganga mwenye sifa kwenye zahanati hiyo na nyingine nne wilayani Chunya.
Kumbuli alidai kuwa chanzo cha tatizo hilo ni uhaba wa watumishi kwenye halmashauri hiyo na kwamba jitihada za kukabiliana na tatizo hilo zinafanyika katika Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
“Tuna changamoto kubwa ya uhaba wa watumishi hasa kwenye sekta ya afya, hali hii inachangiwa na serikali kusitisha kuajiri watumishi wapya ili kupisha uhakiki wa watumishi, lakini punde tu serikali ikianza kuajiri, tunaamini tutaletewa watumishi ambao watatusaidia kupunguza tatizo hili, hata hivyo tatizo la ukosefu wa mganga kwenye zahanati ya Mafyeko linashughuliwa na Ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa na ninaamini litapatiwa ufumbuzi hivi karibuni,” alisema.
Akizungumza na wananchi hao, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, alitoa siku tatu kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, kupeleka mganga mwenye sifa.
Alisema, anatambua changamto ya uhaba wa watumishi kwenye sekta ya afya katika halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya, lakini akamtaka Mganga Mkuu kuangalia mahali penye idadi nzuri kidogo ya watumishi ndani ya mkoa amhamishe mmoja na kumpeleka kwenye zahanati hiyo ili kutatua kero ya muda mrefu ya wananchi hao.



0 comments:
Post a Comment