Thursday, November 17, 2016
Mwenyekiti kortini rushwa kitambulisho cha Taifa
MWENYEKITI wa Mtaa wa Mwangaza katika Halmashauri ya Mji Tarime kupitia Chadema, Abdalah Maindi (53), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya Tarime mkoani Mara akidaiwa kupokea Sh 11,000 kutoka kwa mwananchi Magara Masatu aliyetaka kusainiwa na kugongewa muhuri katika fomu zake za kitambulisho cha Taifa.
Akisomewa shitaka hilo juzi mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Tarime, Amoni Kahimba, Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Martine Makani alidai kuwa Novemba 15, mwaka huu saa tisa mchana katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Nyamisangura Tarime Mjini mwenyekiti huyo alimwomba fedha Sh 11,000 Magembe aliyefika ofisini kwake kupata huduma ya kusainiwa na kugongewa muhuri katika fomu zake za kitambulisho cha Taifa.
Makani alidai kuwa mwenyekiti huyo alidai fedha hizo ndipo asaini na kugonga muhuri.
Mwanasheria huyo wa Takukuru amedai mwananchi huyo aliondoka baada ya kukosa fedha hizo na kufika ofisi za Takukuru na kutoa taarifa na ndipo alipopewa fedha hizo na kuandaa mtego na kufanikisha kukamatwa kwa Maindi baada ya kuzipokea na kusaini fomu zake na kukamatwa akiwa na Sh 11,000 ambazo hazikuwa na stakabadhi yoyote.
Mshitakiwa alikana shitaka hilo huku akidai kuwa ni michango waliojiwekea katika kata yao ya kufanikisha ujenzi wa madarasa.



0 comments:
Post a Comment